Michezo Mingine

Dar Leopards kuumana na Les Gaulois Jumamosi

DAR ES SALAAM:MASHABIKI wa mchezo wa Rugby wanatarajiwa kushuhudia mpambano mkali wikendi hii, wakati wenyeji Dar Leopards watakapowakaribisha Les Gaulois de Nairobi kutoka Kenya.

Pambano hilo litafanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Jumamosi ya Mei 31, 2025.

Akizungumza na SpotiLeo Katibu Mkuu wa Chama cha Rugby Tanzania (TRU), Antony Edward, amesema mechi hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuinua viwango vya mchezo huo Afrika Mashariki.

“Tunatarajia tukio la aina yake. Hii si mechi ya kawaida ni vita ya vigogo wa Rugby wa ukanda huu. Tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia kipute hiki cha kihistoria,” amesema Antony.

Mbali na mechi kuu ya wanaume, kutakuwa pia na onesho la kuvutia la wanawake kupitia timu ya Cheetahs Women’s 7s, watakaoingia uwanjani saa 9:00 alasiri, kabla ya pambano la wanaume kuanza saa 9:30.

Antony pia amethibitisha kwamba Tendai Mtawarira “The Beast” mchezaji wa zamani wa Afrika Kusini waliochukua ubingwa wa Dunia 2019, alipaswa kuhudhuria, hatoweza kufika kufuatia kufutwa kwa hafla hiyo aliyoalikwa awali.

Hata hivyo, ameongeza kuwa hamasa na nguvu za mchezo zitabaki kuwa juu mno.“Ni kweli, The Beast hatoweza kuungana nasi, lakini hiyo haipunguzi chochote kwenye ubora wa tukio. Tunahakikisha mashabiki wanapata burudani ya kiwango cha juu kabisa,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Antony, tukio hili ni fursa ya kipekee kwa Rugby ya Afrika Mashariki kuonesha maendeleo na ushindani wa hali ya juu.

Related Articles

Back to top button