Dar City yavuta mchezaji wa Marekani

DAR ES SALAAM: Klabu ya mpira wa kikapu ya Tanzania, Dar City, imepata nguvu mpya baada ya kumsajili mchezaji mahiri kutoka Marekani, Obadiah Noel, kwa ajili ya kushiriki katika Mashindano ya Ukumbusho wa Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994, yatakayofanyika Kigali kuanzia leo Aprili 23 hadi Aprili 27, 2025.
Noel mwenye umri wa miaka 25, ambaye awali aliichezea klabu ya APR katika michuano ya Afrika ya BAL 2025, ni miongoni mwa wachezaji waliotua Kigali na kikosi cha Dar City.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Rwanda, huenda akawepo katika kikosi kitakachomenyana na timu ya Rwanda ya United Generation Basketball (UGB) siku ya kesho
Katika BAL 2025, Noel alijitokeza kama mmoja wa wachezaji wa kuaminika wa APR kwa uwezo wake mkubwa wa kufunga na uongozi wa timu.
Hata hivyo, hakufanikiwa kuiwezesha APR kufuzu hadi fainali za BAL baada ya kuumia katika michuano ya Kanda ya Sahara iliyofanyika Dakar, Senegal.
Mwaka uliopita, Noel aliichezea APR kwa mara ya kwanza katika nusu fainali ya Mashindano ya Ukumbusho wa Mauaji ya Kimbari, ambapo alifunga pointi 26, rebounds 7 na pasi 3 dhidi ya REG mnamo Novemba 18, 2024.
Sasa anarudi tena kushiriki katika mashindano haya ya heshima, yanayolenga kuwaenzi wanamichezo wa mpira wa kikapu waliopoteza maisha yao katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994. Dar City imepangwa kundi moja na timu ya UGB na Patriots.