Cunha akitathmini kiwango chake United

LONDON: MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Matheus Cunha, amesifu kufufuka kwa klabu hiyo na ushawishi wa meneja Ruben Amorim katika kurejesha makali yake, jambo ambalo limemsaidia kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha Brazil chini ya Carlo Ancelotti, kuelekea Kombe la Dunia la FIFA 2026.
Cunha, mwenye umri wa miaka 26, amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Brazil tangu Ancelotti alipochukua mikoba ya kuinoa timu hiyo mwezi Mei mwaka huu, akipewa jukumu la kuandaa timu hiyo yenye mataji matano ya Dunia kuelekea michuano ya mwakani itakayofanyika Amerika Kaskazini.
Akiwa chini ya Amorim, Cunha ameng’ara kwenye safu ya ushambuliaji ya Manchester United msimu huu na amejumuishwa kwenye vikosi vyote vinne vilivyoteuliwa na kocha Ancelotti, akiamini uwezo wake wa kucheza katika nafasi nyingi umeimarisha nafasi yake kwenye timu ya taifa.
“Kujua kocha ananitegemea kucheza nafasi tofauti ni jambo muhimu. Inanipa wajibu wa kuwa mchezaji mwenye uamuzi na kufanya kazi kwa bidii popote anaponihitaji.” – Cunha aliwaambia waandishi wa habari mjini London, Jumanne.

Cunha alikiri kuwa kurejea kwa mafanikio Manchester United kumechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yake ya sasa katika timu ya taifa, akitafakari maumivu ya kuachwa nje ya kikosi cha Brazil kilichoshiriki Kombe la Dunia 2022 akiwa Atletico Madrid.
“Ni maumivu ambayo yalinifunza mengi, Kukosa nafasi Qatar kuliniumiza, lakini kulinisaidia kukua kifikra. Leo, yale maumivu umekuwa motisha ya mafanikio yangu.” – amesema
Akizungumzia maandalizi ya kuelekea Kombe la Dunia, Cunha amesifu nidhamu na mwelekeo mpya chini ya Ancelotti akisema timu hiyo imekuwa na sura tofauti na wachezaji wamekuwa wakibadilika mara kwa mara na kila mmoja anafahamu malengo ya timu huyo.
Brazil itakabiliana na timu ya taifa ya Senegal katika mchezo wa kirafiki katika Uwanja wa Emirates jijini London Jumamosi.




