
LONDON: GOLIKIPA wa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Thibaut Courtois wa Real Madrid, amesema yuko kamili kuwakabili Washika Mitutu wa jiji la London, Arsenal, katika mchezo wa kukata na shoka wa UEFA Champions League unaotarajiwa kupigwa leo dimbani Emirates jijini London.
Courtois mwenye miaka 32 ameikosa michezo mitatu ya hivi karibuni ya Real Madrid kutokana na majeraha, na sasa amewaambia waandishi wa habari usiku wa kuamkia leo kuwa yuko tayari kwa mchezo huo mkubwa.
“Niko fiti na najihisi vizuri, halikuwa jambo kubwa, lilikuwa suala la kufanya mazoezi tu gym basi, na nimekuwa uwanjani jana tu, kwahiyo najiona fiti kwa 100%,” alisema Courtois.
“Nawaheshimu sana Arsenal, nina marafiki wengi wanaoshabikia Arsenal, najua wanafanya vizuri, wamekuwa wakilikaribia taji la Premier League mara nyingi, wanacheza vizuri na wana wachezaji wenye uzoefu,” aliongeza.
Real Madrid ililazimika kumtumia kinda Fran Gonzalez katika mchezo uliopita walipoteza 2-1 mbele ya Valencia wikiendi iliyopita, baada ya golikipa wao namba mbili Andriy Lunin pia kuwa majeruhi, huku kauli hii ya Courtois ikiwa kama faraja kwa mashabiki wengi wa Real Madrid kuelekea mchezo huo.