Chuchu Hans ataja sababu za kushindwa kufunga ndoa

DAR ES SALAAM:MWIGIZAJI maarufu wa filamu na tamthilia nchini Chuchu Hans, amesema uhusiano wake na mzazi mwenzake Vicent Kigosi ‘Ray’ sio tu haueleweki licha ya kuishi pamoja bali pia, kikwazo Cha wao kushindwa kufunga ndoa ni suala la dini.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari Dar es Salaam Leo baada ya Kusaini mkataba wa miaka mitatu dili la ubalozi wa kampuni ya ujenzi ya Ligae Hardware, amesema utofauti wa dini yeye muislam na mwenzake mkristo ni miongoni mwa mambo yanayoleta mvutano.
Amesema hajui ni lini watafunga ndoa, wanaendelea kuishi pamoja akiwa njiapanda na mzazi mwenzake kwani hana mpango wa kuanzisha mahusiano mapya kwa sasa.
“Nimekuwa kwenye mahusiano zaidi ya miaka kumi. Siri ya kudumu ni kujitambua na kujenga msingi imara wa maisha. Lakini ukiona mtu hashiki mkono wako kwenda mbele, ni lazima ujitathmini,” amesema.
Kuhusu dili alilosaini, amesema kampuni hiyo imekuwa ikimhamasisha kudunduliza fedha kidogo kidogo kwa ajili ya kujenga nyumba yake maeneo ya Kigamboni ambapo mpaka sasa imefikia asilimia 70 na huenda ikakamilika mwakani.
“Nimejenga kwa juhudi zangu mwenyewe. Nimeanzia chini kabisa. Watu wengi hawajui kuwa ujenzi wangu unaungwa mkono na kampuni ya Ligae Hardware waliokuwa bega kwa bega nami. Hakuna kigogo nyuma yangu kama watu wanavyodai,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Ligae hardware Twaha Mruma amesema kupitia kampeni ya Mwanamke na Ujenzi wamekuwa wakihamasisha wanawake kudunduliza fedha kidogo na kufanya ujenzi hivyo, wanaaamini kupitia ushawishi wa Chuchu utasaidia wengine kujiunga kwa ajili ya kujengwa nyumba ya kisasa.