KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Yusufu Chipo amesema maandalizi ya kuikabili Simba katika mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara yataanza rasmi leo jioni na lengo kuu ni kuchukua pointi tatu.
Akizungumza na SpotiLeo leo, kocha huyo amesema anatambua mchezo utakuwa mgumu lakini ushindi katika mchezo huo ni muhimu ili kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi.
“Unajua ni mchezo muhimu halafu hatupo katika nafasi nzuri kwa hiyo huu ni mchezo mgumu lakini tumepanga kuutumia kwa ajili ya kurudisha furaha kwa mashabiki wetu,” amesema Chipo.
Kwa mujibu wa kocha huyo atakachokifanya kwa wachezaji wake ni kuwapa mbinu muhimu zitakazowapa nguvu ya kupambana bila ya kuihofia Simba.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa uwanja wa Mkwakwani Tanga, Desemba 3, Simba ikihitaji kushinda ili kuendelea kuikaribia Yanga inayoongoza ligi.




