Chief Godlove: Pipi Jojo sijamsign, namsaidia kwa upendo

DAR ES SALAAM: Meneja wa msanii wa Bongo Fleva, Grady Godlove ‘Pipi Jojo’, Godlove Mwakibete maarufu kama ‘Chief Godlove’, amefunguka kuhusu uhusiano wake wa kikazi na msanii huyo, akieleza kuwa hana mkataba wowote naye bali anamsaidia kwa upendo.
Akizungumza na Spoti Leo, Chief Godlove amesema watu wengi wamekuwa wakimuuliza iwapo amemsainisha Pipi Jojo katika lebo yake ya muziki, lakini amesisitiza kuwa kwa sasa hakuna mkataba uliosainiwa.
“Watu wengi wananiuliza kama Pipi Jojo kuna mkataba wowote nimefanya naye au nimemsainisha kwenye label, jibu ni hapana. Mambo yote niliyofanya, nimefanya kama baba anavyomsapoti mwanae kufikia ndoto zake. Ni malezi ya baba kwa mwanae. Mawakili wangu hawajapitisha wino,” amesema Chief Godlove.
Ameeleza kuwa tayari amefungua lebo ya muziki kwa ajili ya kusaidia na kufanya biashara ya muziki kimataifa, lakini mpaka sasa bado hajamsainisha msanii yeyote.
“Ni kweli nimefungua label ya muziki kwa ajili ya kusapoti na kufanya biashara ya muziki internationally, siyo local.
“Uwekezaji upo, lakini Pipi bado hajasainiwa, na hadi sasa sijui ni nani atakuwa wa kwanza kusainiwa iwe Pipi au mwingine,” ameongeza.
Chief Godlove pia amefichua masharti ya mkataba wa lebo hiyo endapo Pipi Jojo ataamua kusaini.
“Kama Pipi Jojo atasaini kwenye label, basi asilimia 30 ya mapato yatakuwa yake, na asilimia 70 yatakuwa ya label kwa ajili ya kusimamia kila kitu kinachomhusu. Mkataba ni wa miaka 10,” amesema.
Amehitimisha kwa kusema kuwa tayari kuna video tano za Pipi Jojo ambazo hazijatolewa, na amewataka mashabiki kujiandaa na kazi bora zaidi kutoka kwa msanii huyo.
“Kuna video tano ziko kabatini za Pipi Jojo ni balaaa! Jiandaeni tu,” ameongeza Chief Godlove.




