Charles M’Mombwa aanza na mguu mzuri Ligi Kuu Malta

VALLETA: KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania Charles M’Mombwa, ameonesha makali yake barani Ulaya baada ya kutajwa kuwa mchezaji bora wa mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Malta kati ya Floriana FC dhidi ya Naxxar Lions.
Katika mchezo huo uliochezwa jana Floriana anayocheza M’mombwa iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Katika mechi hiyo ya ufunguzi wa msimu, M’Mombwa alionekana kuwa moyo wa timu, akitawala eneo la kiungo, kusimamia mipangilio na kusaidia kuendesha mashambulizi jambo lililomfanya atajwe kama mchezaji bora wa mechi.
Safari yake ya soka ilianza katika timu za vijana kama Mt Druitt Town Rangers na CCM Academy, kabla ya kujiunga na Macarthur FC mwaka 2020. Mwaka huu 2025, alisaini rasmi na Floriana FC ya Malta kwa msimu wa 2025/26.
Ushindi wa 3–1 dhidi ya Naxxar Lions sio tu uliwaletea Floriana pointi tatu muhimu, bali pia ulidhibitisha haraka thamani ya M’Mombwa kama kiungo mpya aliye na uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko ya maana katika kikosi hicho.