CAF yamfungia Etoo mechi nne na faini juu

RABAT: SHIRIKISHO la Soka Barani Afrika (CAF) limemfungia Rais wa Shirikisho la Soka Cameroon (FECAFOOT), Samuel Eto’o mechi nne, kufuatia matukio yaliyojitokeza katika robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kati ya Morocco na Cameroon.
Kwa mujibu wa uamuzi wa kamati ya nidhamu ya CAF, Eto’o pia, ametozwa faini ya dola 20,000 (takribani Sh milioni 50 )za Marekani, adhabu iliyotokana na mwenendo wake uliotajwa kuwa wa kupitiliza baada ya Cameroon kufungwa mabao 2-0 na Morocco.
Tukio hilo lilitokea Januari 9 mjini Rabat, katika Uwanja wa Prince Moulay Abdellah, ambapo Eto’o alionekana akionesha hasira kali akilalamikia maamuzi ya waamuzi mara baada ya mchezo kumalizika.
Inadaiwa kuwa aliwakabili maofisa wa mashindano mbele ya Rais wa CAF, Patrice Motsepe, na Rais wa Shirikisho la Soka Morocco, Fouzi Lekjaa, kabla ya kuzuiwa na watu waliokuwa karibu naye.
CAF imesema mwenendo huo haukuwa wa kistaarabu na hauendani na maadili ya uongozi wa soka, hali iliyoifanya kamati ya nidhamu kuchukua hatua za haraka dhidi ya nguli huyo wa zamani wa Barcelona na Inter Milan.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka Cameroon (FECAFOOT) limeupinga vikali uamuzi huo, likieleza kuwa haukuwa na maelezo ya kina yanayoeleza makosa aliyotenda Eto’o.
Kupitia taarifa rasmi, FECAFOOT imesema adhabu hiyo imetolewa kwa haraka bila mchakato wa haki na imetangaza kuwa itachukua hatua za kisheria kupinga uamuzi wa CAF.
Shirikisho hilo pia limethibitisha kuwa linasimama imara kumuunga mkono Rais wake, likisisitiza kuwa Eto’o alikuwa akitetea maslahi ya soka la Cameroon.
Hatua hiyo ya CAF imezua mjadala mkubwa barani Afrika, huku wachambuzi wa soka wakitofautiana kuhusu uzito wa adhabu hiyo dhidi ya mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea barani Afrika.




