Bwire: Yanga walituchanganya, Dube ni mwanariadha

DAR ES SALAAM : Ofisa Habari wa JKT Tanzania, Masau Bwire, amesema kasi na mbio za mshambuliaji Dube zimewapa wakati mgumu vijana wake, akidai ni kama ameandaliwa rasmi kuwa nwanariadha kutokana na namna alivyokuwa akikimbia kuwania mipira mirefu.
Kauli hiyo ni baada ya timu yake kupoteza kwa kichapo cha mabao 5-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC jana.
Bwire amesema wapinzani wao walibadili kabisa mtindo wa kawaida wa soka la pasi na kuamua kucheza mipira mirefu ya kushtukiza iliyokuwa inamtafuta moja kwa moja Dube.
“Walikuwa wakifika katikati hawatizami mtu, wanapiga mpira mrefu. Dube mtaalam wa mbio, nadhani wamemfundisha rasmi kwamba wewe ni riadha sasa hivi fukuza kweli kweli, kimbia,” amesema Bwire.
Bwire amesema kuwa JKT Tanzania ilijipanga kucheza mpira wao wa pasi uliopangiliwa na unaovutia mashabiki, lakini wakakutana na aina ya soka la mbio ambalo hawakulitegemea.
“Sisi tulijipanga kucheza mpira wetu wa pasi, uliopangwa kwa programu maalumu. Lakini wenzetu wamekuja na mpira wa mbio, wanatanguliza halafu mnafukuzana kama sungura anayekimbizwa na mbwa mwenye njaa. Vijana wetu hilo limewachanganya kidogo,” alifafanua.
Hata hivyo, Bwire amesisitiza kuwa pamoja na changamoto hiyo, malengo ya JKT Tanzania bado yapo hai na wanaamini watarejea katika ubora wao.




