Muziki

Britney Spears auza muziki wake kwa Sh Bilioni 26

LOS ANGELES:MWANAMUZIKI maarufu wa pop duniani, Britney Spears, ameripotiwa kuuza katalogi yake yote ya muziki kwa kampuni huru ya uchapishaji wa muziki ya Primary Wave kwa makubaliano yanayokadiriwa kufikia Sh26 bilioni saw ana dola milioni 200.

Kwa mujibu wa BBC, dili hilo lilikamilishwa mwishoni mwa mwezi Desemba na linaweka alama kubwa ya kifedha kwa msanii huyo mwenye umri wa miaka 44, ambaye amedumu katika tasnia ya muziki kwa zaidi ya miongo miwili.

Kupitia hatua hiyo, Spears anaungana na orodha ya wasanii wakubwa waliouza haki za kazi zao za muziki katika miaka ya karibuni, akiwemo Bruce Springsteen, Justin Bieber na Shakira.

Primary Wave, iliyoanzishwa na Lawrence Mestel, ni moja ya kampuni zenye ushawishi mkubwa katika usimamizi wa haki za muziki. Kampuni hiyo pia inasimamia haki za wasanii na makundi mashuhuri kama Prince, Whitney Houston na Nirvana.

Britney Spears alianza kung’ara mwaka 1999 baada ya kuachia wimbo wake wa kwanza …’Baby One More Time’ ambao ulimpa umaarufu wa kimataifa. Tangu wakati huo, ameuza zaidi ya nakala milioni 150 za muziki wake duniani na kutoa vibao vilivyotikisa chati kama ‘Toxic’ na ‘Gimme More’.

Hata hivyo, safari yake imekuwa na mafanikio pamoja na misukosuko mikubwa ya maisha binafsi. Mwaka 2021 aliachiliwa rasmi kutoka katika mfumo wa kisheria wa ulezi (conservatorship) uliodumu kwa miaka 13, uliompa baba yake mamlaka ya kusimamia fedha na maamuzi ya maisha yake binafsi.

Mwaka 2023, Spears alielezea kwa kina maisha yake katika kitabu chake cha kumbukumbu ‘The Woman in Me’. Aidha, aliyekuwa mume wake, Kevin Federline, naye alitoa kitabu chake ‘You Thought You Knew’ mwishoni mwa mwaka 2025.

Licha ya dili hilo kubwa la kibiashara, mashabiki wanaweza kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kusikia muziki mpya kutoka kwake. Mapema mwaka 2024, Spears alitangaza kuwa “hatarudi tena katika tasnia ya muziki,” huku kazi yake ya mwisho kuwa wimbo wa ushirikiano aliyofanya na Elton John mwaka 2022.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button