Muziki

Britney ahofia kuwekwa chini ya uangalizi

CALIFORNIA: MSANII maarufu wa muziki wa pop, Britney Spears anaripotiwa kukumbwa na hofu kubwa kufuatia kukamatwa kwake kwa tuhuma za kuendesha gari akiwa amelewa, huku akihofia kurejea katika kipindi cha maisha ya uangalizi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vya karibu, nyota huyo mwenye umri wa miaka 44 anadaiwa kuwa katika hali ya wasiwasi mkubwa akihofia kuwa huenda akapelekwa kwenye kituo cha matibabu ya uraibu (rehab), kufungwa jela, au hata kurejeshwa chini ya uangalizi maalum wa kisheria (conservatorship).

Taarifa zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea karibu na nyumbani kwake mjini Thousand Oaks, baada ya kudaiwa kuendesha gari kwa kuyumbayumba barabarani.

Baada ya kukamatwa, alipelekwa hospitali kwa uchunguzi kabla ya kuwekwa mahabusu kwa muda mfupi na kuachiwa huru saa chache baadaye.

Aidha, mamlaka zinaendelea kuchunguza dawa aina ya Adderall iliyokutwa akiwa nayo ili kubaini iwapo ilikuwa halali au la.

Tukio hili linakuja miaka minne baada ya mahakama kumaliza rasmi uangalizi wa kisheria uliokuwa ukidhibiti maisha na mali za Spears kwa zaidi ya miaka 13 hatua iliyokuja kufuatia kampeni kubwa ya umma iliyoungwa mkono na mashabiki wake duniani kote kwamba arudi tena kuwa huru baada ya kubadirika kitabia.

Chanzo kimoja kinasema kuwa kwa sasa msanii huyo ana hofu ya kupoteza tena uhuru wake alioupigania kwa muda mrefu. Inaelezwa kuwa kumbukumbu za maisha chini ya uangalizi huo zilikuwa za kuumiza na zenye vikwazo vingi kwake, jambo linalomfanya ashindwe kuvumilia kila anapoona uwezekano wa kuwa kizuizini tena.
Iwapo atapatikana na hatia, Britney Spears anaweza kukumbana na adhabu ikiwemo kufungiwa kuendesha gari, au hata kifungo jela endapo makosa yatakuwa makubwa zaidi.

Wakati mashabiki wake wakiendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya sakata hili, mustakabali wa nyota huyo unabaki kuwa wa sintofahamu, huku hofu ya kupoteza uhuru wake ikitajwa kuwa changamoto kubwa inayomkabili kwa sasa.

Related Articles

Back to top button