Kuogelea

BMT kugharamia wachezaji 20 mashindano ya Dunia

DAR ES SALAAM: Baraza la Michezo la Taifa ‘BMT,’ limegharamia wachezaji 20 wa ngumi na Kabadi kwa ajili ya kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Dunia.

Kati ya idadi hiyo watano ni mabondia wa kike wa Timu ya Taifa ya Ngumi za Ridhaa na 15 wa mchezo wa Kabadi.
Kwa mujibu wa taarifa ya BMT leo Ijumaa, Februari 28, 2025, Katibu Mtendaji wa BMT Neema Msitha na viongozi wa Chama cha Ngumi za Ridhaa ‘BFT’ na wa mchezo wa Kabadi wamekutana kwa nyakati tofauti kujadili maandalizi ya timu hizo zinazotarajia kwenda nchini Serbia na Uingereza kushiriki mashindano hayo.

Wachezaji watano wa ngumi wanatarajia kwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano ubingwa wa Dunia wanawake yanayotarajia kutimua vumbi kuanzia Machi 3 hadi 17, mwaka huu katika mji wa Nis nchini Serbia wakati timu ya Taifa ya mchezo wa Kabadi itaiwakilisha nchi katika mashindano ya Kombe la Dunia yatakayofanyika Machi 15, mwaka huu kwenye mji wa Birmingham, Uingereza.

Msitha amewataka viongozi wa vyama vyote vya michezo vya taifa kuusoma mwongozo wa Serikali wa kuzisaidia timu za taifa.

“Serikali kupitia BMT itazisaidia timu kwa asilimia 25 tu pale inapowezekana huku vyama vyenyewe vikitakiwa kuchangia kwa asilimia 75, hivyo viache kuitegemea serikali peke yake,”amesema.
Mwisho

Related Articles

Back to top button