Africa

Beki Mamelodi aapa ‘kuwaua’ Pyramids mapema

PRETORIA: BEKI wa Mamelodi Sundowns, Mothobi Mvala amesema hawawezi kuruhusu kujisahau au kupungukiwa na umakini na lazima “wamalize mchezo” mapema katika mechi ya marudiano ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Africa jumapili ugenini dhidi ya klabu ya Pyramids ya Egypt.

Pyramids ndio wenye faida kubwa baada ya kufanikiwa kufunga bao kwenye Uwanja wa nyumbani wa Mamelodi Sundowns wa Loftus wikendi iliyopita na kuondoka mjini pretoria wakiwa na faida hiyo ya goli la ugenini lenye thamani kubwa katika michuano ya CAF sekunde chache kabla ya kipyenga cha mwisho cha sare ya 1-1.

Mamelodi Sundowns sasa watalazimika kutumia nguvu ya ziada ugenini na kushinda kwa tofauti ya bao moja kwenye matokeo ya jumla huku wakizuia wasifungwe bao jingine ili waweze kutwaa ubingwa wa kombe hilo katika Uwanja wa Juni 30 jijini Cairo na Mvala anaamini njia pekee ya kufanya hivyo ni kuwanyima Pyramids nafasi na kufanya chochote kwenye lango lao.

“Tulianza mechi ya kwanza sana, na tukafanikiwa kuzuia krosi zao, ilikuwa ni dakika za lala salama ambapo tulipoteza umakini. Nadhani tunapaswa kuua mchezo huu mapema, na ili kuua mchezo, tunahitaji kufunga mabao mengi,” alisema Mvala kwenye mahojiano na SABC

“Tunawahitaji sana wachezaji wakongwe waje kwenye tukio hili hasa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ili kuwahamasisha vijana kujitoa. Tumeshawahi kucheza Pyramids kule Cairo, na ninaamini kwa sababu hawana mashabiki wengi, hiyo inaweza kuwa ni faida kwetu,” aliongeza Mvala.

Katika mchezo wa mkondo wa kwanza Wachezaji wa Mamelodi walionekana kuchanganyikiwa baada ya kuruhusu Pyramids kurejesha bao dakika za usiku hata hivyo, Mvala anasisitiza kuwa wana matumaini, baada ya kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza tangu 2016 mwaka huu ni mwaka wao hasa ukizingatia uzoefu walionao katika michuano hiyo. Mechi hiyo itapigwa Jumapili Juni 1, saa 2 usiku Afrika Mashariki.

Related Articles

Back to top button