Barker: hatukutarajia matokeo ya sare

MWANZA: KOCHA Mkuu wa Simba, Steven Barker, amesema sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba haikuwa matokeo waliyoyatarajia, kwani kila wanapoingia uwanjani lengo lao ni kushinda na kupata pointi tatu.
Akizungumza baada ya mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza jana Barker amesema walijua mapema kuwa mchezo huo usingekuwa mwepesi kwa sababu Pamba ni timu imara na ngumu kufungwa, huku akieleza kuwa kabla ya mechi hiyo walikuwa wamepoteza michezo mitatu pekee, jambo linaloonesha ubora wao.
Amesema kuwa Pamba tayari ilionesha uwezo wake katika mchezo dhidi ya Azam, hivyo Simba walihitaji kufanya vizuri zaidi katika baadhi ya maeneo, hususan kwenye eneo la ushambuliaji la mwisho.

Kocha huyo amesema changamoto ya kukosekana kwa baadhi ya washambuliaji kutokana na majeraha na adhabu za kusimamishwa, ilipu,nguza chaguo la kufanya mabadiliko ambayo yangeweza kuongeza nguvu mbele.
Pamoja na kutoridhishwa na sare hiyo, Barker amesema Simba bado inaendelea kuonesha dalili za kuwa kwenye mwelekeo sahihi na kasi nzuri ya maendeleo, huku akiitaja matokeo hayo kama kikwazo kidogo ambacho ni sehemu ya safari ya timu.
Barker amesema sasa wanageukia michezo miwili ya nyumbani inayofuata, akisisitiza kuwa jambo muhimu zaidi ni namna watakavyojibu baada ya matokeo hayo.



