Ligi Kuu

Barker: Hakuna mchezo mwepesi Ligi Kuu

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steven Barker, amesema kikosi chake kina hamasa kubwa kurejea katika michezo ya Ligi Kuu baada ya kumaliza ratiba ya michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF).

Barker amesema tayari timu imerejea mazoezini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo dhidi ya KMC unaotarajiwa kuchezwa kesho jioni, akisisitiza kuwa kila mchezo wa ligi una umuhimu mkubwa kwao.

“Kwa sasa tuko nyuma kwa idadi ya mechi tulizocheza ukilinganisha na wapinzani wetu, hivyo ni muhimu kuhakikisha tunapata pointi zote tatu ili kuendelea kusalia karibu na kilele cha msimamo wa ligi,” amesema Barker.

Ameongeza kuwa licha ya kuwaheshimu wapinzani wao, wanatambua wazi kuwa hakuna mchezo mwepesi katika ligi, lakini amefurahishwa na kiwango cha kujituma kilichooneshwa na wachezaji wake.

“Ninaamini timu inaendelea kukua kutoka mchezo mmoja hadi mwingine. Tunazidi kuwa imara. Baadhi ya viwango tulivyovionesha hivi karibuni vikidumishwa, tayari tumeweka msingi mzuri,” amesema.

Kocha huyo pia amesema wachezaji wapya wameanza kuzoea mazingira ya timu na kuungana vyema na wenzao, hali inayosaidia Simba kuanza kujenga mwelekeo mzuri na kupata kasi (momentum), hasa baada ya mechi ngumu za Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Tunaangalia mbele, tuna matumaini makubwa na tunasubiri kwa hamu mchezo wa ligi wa kesho,” amehitimisha Barker.

Related Articles

Back to top button