Baba Ali Kamwe: Wakati wa Ali Kamwe Kuoa Umefika, Aoe

DAR ES SALAAM: BABAwa Msemaji wa Yanga, Shaban Kamwe, amemshauri mwanawe Ali Kamwe kuwa muda wake wa kuoa umefika, kwani kilichokuwa kinamkwamisha (nyumba kwa mama yake), tayari ameshatimiza.
Mzee Kamwe amesema “Mwenyewe alishasema kilichokuwa kinamkwamisha kuoa, na tumekiona. Amekwishamtimizia mama yake, sasa namshauri asisubiri hadi mama yake amwambie aoe. Muda umefika, ametimiza alichotakiwa kutimiza, sasa aoe”.
Mzee huyo amemtaka Ali Kamwe asiwe na hofu ya kuoa kwa sababu alishawahi kuoa, ingawa ndoa yake ya awali haikudumu. Hata hivyo, amemtia moyo kuwa sasa amekomaa kifikra na kiakili, hivyo anaweza kuwa mume bora tofauti na alivyokuwa hapo awali.
“Ali Kamwe alishaoa, lakini ndoa yake haikudumu kwa sababu hakuwa mwanaume bora, bali alikuwa bora mwanaume. Ila asiogope kujaribu tena, kwani hata mitume walioa na kuacha. Sasa ni wakati wake wa kuoa, sina kingine cha kumwambia mtoto wangu Ali zaidi ya hilo,” amefafanua Mzee Kamwe.
Ameeleza kuwa ndoa ya mwanawe ilivunjika kwa sababu yeye na mke wake wa awali hawakuwa wanandoa bora, bali walikuwa bora ndoa.
“Wote walikuwa hovyo. Ali Kamwe hakuwa mwanaume bora, alikuwa bora mwanaume, na mkewe pia alikuwa bora mke, siyo mke bora, ndiyo maana ndoa yao haikudumu. Lakini kwa sasa naamini yupo sawa na anaweza kuwa mwanaume bora. Mama yake yupo karibu naye na atakuwa mshauri mzuri katika ndoa yake kama ataoa,” amesema Mzee Kamwe.
Aidha, Mzee Kamwe alijipongeza kwa kudumu katika ndoa kwa miaka 34, akisisitiza kuwa mafanikio ya ndoa yanahitaji kujitoa kwa kila upande.
“Nimedumu katika ndoa kwa miaka 34 na mke wangu. Sisi si wakamilifu, lakini mmoja alikubali kumfanya mwenzake kuwa bora, ndiyo maana tumeweza kuendelea. Ni kazi ya mwanaume na mwanamke kumfanya mwenza wake kuwa bora, lakini kama wote hawatakuwa na juhudi hizo, hakuna ndoa itakayodumu,” amesema.