
MIAMBA ya soka nchini klabu ya Azam leo imeshindwa kutamba ugenini baada ya kufungwa bao 1-0 na maafande wa Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliopigwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Mshambuliaji Jeremiah Juma ndiye aliyewapeleka korokoroni Azam kwa bao hilo pekee dakika ya 46 baada ya shambulizi lililoelekezwa lango mwa klabu hiyo ya Dar es Salaam.
Hicho ni kipigo cha kwanza kwa Azam ambayo kwa sasa imeshuka hadi nafasi ya sita kutoka nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kabla ya mchezo huo huku Tanzania Prisons ikipanda hadi nafasi ya nane ikifikisha pointi nane.
Mchezo huo ulianza kwa timu zote mbili kushambuliana kwa zamu lakini Azam ndio waliotengeneza nafasi nyingi ambazo washambuliaji wao walishindwa kuzitumia na hadi mapumziko timu hizo hazifungana.