Nyumbani

Azam, Yanga yasaka historia mpya Mapinduzi Cup

PEMBA:MABINGWA watarajiwa wa Kombe la Mapinduzi 2026 watapatikana leo jioni saa 10:30, wakati vigogo wa soka nchini Azam FC na Yanga SC watakapovaana kwenye fainali ya michuano hiyo itakayopigwa katika Uwanja wa Gombani, Pemba.

Ni fainali yenye historia yake, kwani kwa mara ya kwanza tangu Kombe la Mapinduzi lilipoanza kushirikisha timu kutoka nje ya Zanzibar, Azam na Yanga zinakutana hatua ya mwisho ya mashindano hayo, jambo linaloipa fainali hiyo mvuto wa kipekee kwa mashabiki wa soka nchini.

Azam FC inaingia kwenye mchezo huo ikiwa klabu iliyofanikiwa zaidi katika historia ya Kombe la Mapinduzi, baada ya kutwaa mataji matano katika fainali saba ilizowahi kushiriki. Mabingwa hao wa zamani walitwaa mataji hayo mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019, na leo watakuwa wakisaka taji lao la sita ili kuendelea kuimarisha rekodi yao.

Kwa upande wa Yanga, klabu hiyo yenye mashabiki wengi nchini imeshinda mataji matatu ya Kombe la Mapinduzi, yaliyopatikana mwaka 2007, 2011 na 2021.

Wananchi wanaitazama fainali hiyo kama fursa ya kuongeza taji la nne na kurejea kileleni baada ya miaka kadhaa bila kulitwaa kombe hilo.

Fainali hiyo pia inatarajiwa kuwa vita ya makocha, ikiwakutanisha Florent Ibenge wa Azam FC na Pedro Goncalves wa Yanga.

Licha ya uzoefu mkubwa walionao katika soka la Afrika, ni mara ya kwanza kwa makocha hao kuiongoza timu zao katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, kila mmoja akiwa na dhamira ya kutwaa taji lake la kwanza kwenye mashindano hayo.

Hata hivyo, Yanga itakosa huduma ya kiungo Mohamed Damaro, ambaye atakuwa nje ya uwanja kutokana na adhabu ya kadi nyekundu aliyopata katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Singida Black Stars, hali inayompa changamoto Goncalves kupanga safu yake ya kati.

Kwa uzito wa fainali hiyo, rekodi za kihistoria na ubora wa vikosi vya timu zote mbili, macho na masikio ya mashabiki wa soka yatakuwa Uwanja wa Gombani, kusubiri nani ataibuka mshindi na kuandika ukurasa mpya katika historia ya Kombe la Mapinduzi.

Related Articles

Back to top button