Azam FC watoa kauli ishu ya Feitoto na wenzie!

DAR ES SALAAM: UONGOZI wa klabu ya Azam FC umeweka wazi msimamo wake kuhusu wachezaji wao kuhusishwa na usajili wa kwenda timu nyingine na wamesisitiza kuwa wako tayari kufanya mazungumzo na klabu yoyote ambayo inahitaji huduma ya mchezaji aliye chini ya mkataba wao.
Kauli hiyo imekuja kufuatia taarifa zinazosambaa kwamba baadhi ya wachezaji wa timu hiyo, akiwemo beki wa kushoto Pascal Msindo, wanawaniwa na klabu ya Simba, Yanga pamoja na timu kadhaa kutoka Afrika Kusini.
Msindo ambaye ni miongoni mwa wachezaji waliocheza kwa kiwango kizuri msimu huu, amekuwa kwenye rada ya klabu hizo kufuatia uwezo wake wa kulinda na kushambulia.
Msemaji wa Azam FC, Hashim Ibwe alieleza kuwa mpaka sasa klabu hiyo haijapokea ofa rasmi wala barua yoyote ya kutaka kumsajili Msindo, kuwa taarifa nyingi zinazohusu wachezaji kuhamia timu nyingine zinaibuka kipindi hiki cha mwisho wa msimu, na nyingi hazina ukweli wa moja kwa moja.
“Hiki kipindi cha mwisho wa msimu kuna taarifa nyingi hasa wachezaji kuhusishwa na timu moja kwenda nyingine kwa ajili ya usajili. Azam FC hatujapokea ofa yoyote rasmi kuhusu Msindo au mchezaji mwingine. Kama kuna klabu inahitaji huduma ya mchezaji wetu, basi milango ipo wazi,” amesema.
Ibwe amesisitiza kuwa klabu yenye nia ya dhati inapaswa kuwasiliana moja kwa moja na uongozi wa Azam FC kwa njia rasmi ili kufanya mazungumzo ya kibiashara.
“Mtendaji wetu Mkuu, Abdulkarim Amin ‘Popat’, alikwishaeleza wazi kuwa Azam FC haimzuii mchezaji kuondoka endapo kutakuwa na ofa sahihi na ya kibiashara. Waje mezani tuzungumze,” ameongeza Ibwe.
Azam FC imekuwa na msimamo wa kitaaluma kuhusu uhamisho wa wachezaji wao kwa miaka ya karibuni, Ibwe amesisitiza umuhimu wa taratibu rasmi za uhamisho na kuheshimu mikataba ya wachezaji.