EPL

Arteta aendelea kumtetea Gyökeres

LONDON: KOCHA wa Arsenal Mikel Arteta ameendelea kuutetea ubora wa mshambuliaji Viktor Gyökeres, akisema ana imani kubwa kwamba staa huyo wa Sweeden atafunguka licha ya mwanzo mgumu tangu kuwasili Emirates.

Gyökeres, aliyeng’ara kwa kufunga mabao 54 akiwa Sporting msimu uliopita, ametikisa nyavu mara sita tu katika mechi 18 tangu kusajiliwa kwa paundi milioni 64, huku akiwa na bao moja tu la Premier League tangu Septemba.

Pamoja na ukame huo, Arsenal bado wapo kileleni mwa msimamo wa EPL kuelekea mchezo wa Jumamosi dhidi ya Wolverhampton Wanderers, ingawa kipigo cha dakika za mwisho dhidi ya Aston Villa wikiendi iliyopita kilipunguza pengo la pointi dhidi ya Manchester City na Villa wanaofukuzia kwa karibu.

Arteta amesema changamoto za Gyökeres zinatokana pia na mazingira, majeraha na ukosefu wa maandalizi ya kabla ya msimu yaani Pre-season.

“Tunapaswa kumweka mchezaji katika mazingira bora ili ajitume na kufikia uwezo wake. Kuna majukumu maalum ndani ya mfumo wetu yanayotakiwa kutekelezwa, Kabla ya jeraha alikuwa kwenye kiwango kizuri. Hakufanya pre-season, na sasa anaanza kupata mwendo tena. Magoli yatakuja, na tutafurahi naye sana” – amesema Arteta.

Arsenal wanaimarika pia na kurejea kwa Gabriel Jesus, aliyepata dakika zake za kwanza msimu huu katika ushindi wa 3-0 wa Ligi ya Mabingwa ulaya dhidi ya Brugge Jumatano usiku.

“Tunajua ubora wake. Kama akicheza kama alivyofanya siku ile, basi ni lazima apiganie nafasi ya kuanza,” – Arteta aliongeza.

Wolves, ambao hawajashinda mechi yoyote katika michezo 15 ya mwanzo, wanaonekana tayari wakiwa kwenye hatihati ya kushuka daraja hali ambayo inawapa Arsenal nafasi nzuri ya kurejea kwa kasi kwenye mbio za ubingwa.

Arteta ameweka wazi kuwa kufikisha pointi 90 au zaidi ndicho kiwango kitakachohitajika msimu huu kwa bingwa wa Ligi hiyo inayofuatiliwa zaidi ulimwenguni.

Related Articles

Back to top button