EPLKwingineko

Arsenal yamaliza kwa Rice

‘WASHIKA mtutu’ wa London, Arsenal imethibitisha kumsajili kiungo wa England Declan Rice kutoka West Ham United ‘Wagonga Nyundo’ kwa pauni milioni 100 sawa na shilingi bilioni 304.3 pamoja na nyongeza ya pauni milioni 5.

Tangazo hilo la Arsenal limekuja baada ya Rice mwenye umri wa miaka 24 kutoa barua ya wazi kwa mashabiki wa ‘Wagonga Nyundo’ hao akielezea jinsi gani uamuzi wa kuondoka klabu hiyo ulivyokuwa mgumu.

Rice amehamia Arsenal baada ya kuiongoza West Ham kutwaa Kombe la Ligi ya Conference msimu uliopita.

“Nimekuwa nikiitazama Arsenal kwa misimu kadhaa iliyopita na mwenendo wao. Msimu uliopita ulikuwa bora kwa Arsenal, ikizifunga kila timu isipokuwa Manchester City,” amesema Rice.

Akielezea usajili wa mchezaji huyo Kocha wa Arsenal Mikel Arteta amesema:” Ni mchezaji mwenye uwezo wa hali ya juu, ambaye amekuwa akicheza kwa kiwango cha juu kwenye Ligi Kuu na England kwa misimu kadhaa sasa.”

Rice ni mchezaji wa tatu kusajiliwa Arsenal majira haya ya joto baada ya Kai Havertz aliyekuwa Chelsea kwa pauni milioni 65 na beki wa Uholanzi Jurrien Timber akitokea Ajax kwa ada inayoweza kuongezeka hadi pauni milioni 38.5.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button