Argentina vs Croatia: Nusu fainali ya kufa, kupona
NUSU fainali ya kwanza ya michuano ya Kombe la Dunia inapigwa leo kati ya Argentina na Croatia.
Mchezo huo wa kukata na shoka utafanyika uwanja wa Lusail uliopo eneo la Al Daayen katika mji mkuu wa Qatar, Doha.
Mwamuzi wa kati katika mchezo huo ni Daniele Orsato wa Italia akisaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Ciro Carbone huku mwamuzi msaidizi namba mbili akiwa Alessandro Giallatini.
Kufika hatua hiyo Argentina imeitoa Uholanzi kwa mikwaju ya penalti wakati Croatia imetoa Brazil pia kwa mikwaju ya penalti katika robo fainali.
Katika michezo mitano iliyopita kati ya timu hizo Argentina imeshinda dhidi ya Croatia Komba la Dunia 1998 kwa bao 1-0 wakati Croatia imeshinda dhidi ya Argentina michuano ya 2018 kwa mabao 3-0.
Kwa upande wa michezo ya kirafiki Argentina imeshinda mara moja, Croatia imeshinda mara moja na timu hizo zimetoka suluhu mara maoja.
Kwa nahodha wa Argentina Lionel Messi hiyo itakuwa michuano yake ya mwisho ya Kombe la Dunia.




