La Liga

Ancelotti hana ‘presha’ na kibarua chake

MADRID, Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amepuuzilia mbali tetesi za yeye kuondoka klabuni hapo na kutimkia Brazil ambako anatajwa kuhitajika kuifundisha timu ya taifa hilo iliyotimua kocha hivi karibuni, baada ya tetesi hizo kuenea kwenye vyombo mbalimbali vya Habari nchini Spain.

Tetesi za kocha huyo kutimka zilianza kuibuka mara tu baada ya Real Madrid kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Pamoja na kuonekana hawapo katika mbio za Ubingwa wa LaLiga baada ya kuwa nyuma ya vinara na mahasimu wao FC Barcelona kwa pointi 4. Tetesi hizo pia zinamtaja kocha wa Bayer Leverkusen Xabi Alonso na meneja wa zamani wa Liverpool Juergen Klopp kama warithi wake.

Alipoulizwa na waandishi wa Habari kama anahisi presha yeyote juu ya hilo Ancelotti amesema hana presha kwakuwa uongozi wa klabu hiyo unafahamu fika kinachoendelea klabuni hapo msimu huu.

“Klabu inajua mwaka huu ni mgumu kuliko mwaka uliopita, magumu tunapambana nayo Pamoja na mazuri tunaendelea nayo. Nina furaha sana sana kunaweza kuwa na presha lakini ndivyo mambo yalivyo siku zote”

“Unapoona uko karibu na mafanikio stress kuongezeka ni kawaida lakini kwangu hainisumbui natumia kama kichocheo, inanipa nguvu zaidi za kusonga mbele. Kuna mengi ya kufikiria kwa sasa hilo si mojawapo kwakuwa nikiamka asubuhi naona mambo sawa” alijibu

Real bado wanafukuzia kutimia kwa malengo yao wakiwa nafasi ya pili kwenye ligi nyuma ya Barca kwa pointi 4 na watakutana nao tena kwenye fainali ya Copa del Rey wikiendi hii lakini kabla watakutana na Getafe kesho bila Kylian Mbappe na Ferland Mendy.

Related Articles

Back to top button