Alonso achukua somo kipigo cha PSG

EAST RUTHERFORD, Baada ya kuvurumishwa nje ya Michuano ya kombe la Dunia la Klabu hatua ya nusu fainali kwa aibu ya mabao 4-0 na Mabingwa wa Ulaya PSG Meneja wa Real Madrid Xabi Alonso amesema kikosi chake kimejifunza kutokana na michuano hiyo na kitaanza kujijenga upya kuanzia mwanzo msimu ujao.
Kukosekana kwa beki mpya Dean Huijsen anayetumikia adhabu na Trent Alexander-Arnold aliye majeruhi kulimfanya Alonso ambaye alianza kuinoa Madrid wiki chache zilizopita aonekane wazi kuishiwa mbinu na kurejea kwenye safu ya ulinzi ya watu wanne badala ya watano iliyowasaidia kujilinda vyema katika michezo ya awali.
Mabadiliko hayo ya kimbinu yalimfanya mshambuliaji wake mkubwa kwenye michuano hiyo Gonzalo Garcia aanze sambamba na mshambuliaji nyota Kylian Mbappe ambaye alirejea kwa nguvu zote kwenye kikosi cha kwanza baada ya kukosa mechi za awali kutokana na kuumwa lakini mbinu hiyo haikufua dafu.
“Tulikuwa nyuma kwa mabao mawili tulipotea na hatukuweza kujipata haraka. Kilikuwa kipigo cha maumivu sana lakini sote ni mashahidi na lazima tukubali hatukuwa bora kabisa leo”
“Tulikuwa na mapungufu katika baadhi ya maeneo. wakati mwingine ni vizuri kuona makosa mapema ili ujue cha kufanya siku zijazo. Tunaanza zama mpya baada tu ya mapumziko tukiwa na akili mpya, Tunataka kujenga timu ambayo inacheza pamoja na tunapaswa kuanza kila kitu upya msimu ujao.” – Alonso alisema.
Paris St Germain walitumia haraka udhaifu wa safu ya ulinzi ya Real Madrid kwa kupachika mabao mawili hraka haraka katika dakika tisa za mwanzoni huku timu hiyo ya LaLiga ikionekana kuzidiwa na kasi ya kimbunga ya vijana wa Paris.
Real Madrid hawakuonesha mabadiliko yoyote ya maana kipindi cha pili huku Alonso akiwaambia waandishi wa habari kwamba aliamini walipata nafasi za kufunga na kubadilisha mchezo laini wachezaji wake hawakuzitumia.