World Cup

Afariki kwa furaha ya ubingwa Argentina

KIJANA mmoja wa Misri amefariki dunia kutokana kile kinachojulikana kuwa “ugonjwa wa moyo wenye furaha” wakati akishangalia katika jiji la Cairo baada ya Argentina kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia.

Ripoti zimesema Mostafa Aal aliangalia mchezo wa fainali kati ya Argentina na Ufaransa akiwa kwenye mgahawa katikati ya Cairo pamoja na marafiki zake na alipowasili nyumbani alituma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akimsifu Lionel Messi wa Argentina akielezea kwamba “ilikuwa siku bora zaidi katika maisha yake.”

Baada ya tu ya kutuma ujumbe huo kijana huyo alizimia baada ya kupata mshtuko wa moyo na kupelekwa hospitali ya karibu ambako alifariki dunia.

Daktari wa Moyo wa Misri Gamal Shaaban kupitia mtandao wa Facebook amesema: “Inabidi tujifunze somo kutokana na kile kilichotokea, hatutakiwi kutia chumvi katika kueleza huzuni au furaha yetu.”

Argentina imetwaa ubingwa wa Kombe la Dunia kwa mara ya tatu baada ya kuifunga Ufaransa kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya sare ya mabao 3-3 hadi muda wa nyongeza.

Messi aliibuka mchezaji bora wa michuano hiyo wakati Kylian Mbappé wa Ufaransa amekuwa mfungaji bora.

Related Articles

Back to top button