Abigail Chams atoa neno BET Awards

MSANII wa muziki Abigail Chamungwana, maarufu kama Abigail Chams, ameonesha kuguswa na kufurahishwa na sapoti kubwa aliyoipata kutoka kwa Watanzania na mashabiki wa Afrika Mashariki kufuatia ushiriki wake kwenye tuzo za BET.
Abigail alikuwa mwakilishi pekee kutoka Afrika Mashariki aliyeteuliwa kuwania tuzo ya Best International Act kwenye BET Awards 2025. Ingawa hakufanikiwa kuchukua tuzo hiyo, upendo na mshikamano kutoka kwa mashabiki wake haujapungua hata baada ya tukio hilo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Abby alipost ujumbe wa shukrani uliosomeka:
“Hii imekuwa sura ya kuvutia sana. Nimeguswa kwa dhati na upendo na msaada niliopokea kutoka kwa nchi yangu na hata zaidi. Nasonga mbele nikiwa na furaha moyoni na moto rohoni, huu ni mwanzo tu.”
Mashabiki wake na wadau wa muziki wameendelea kumpongeza kwa hatua hiyo kubwa, wakimtia moyo kuendelea kupigania mafanikio yake kimataifa.




