Tambaza U17 mabingwa ligi ya DRFA

DAR ES SALAAM:TIMU ya mpira wa miguu ya Tambaza Youth wametwaa ubingwa wa Ligi ya vijana ya U 17 ya Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kwa kumfunga Tandika United, mchezo uliochezwa uwanja wa Bandari, Tandika.
Tambaza Youth wametwaa ubingwa huo kwa ushindi kwa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya TandikaUnited, baada ya kutamatika dakika 90 kwa sare ya bao 1-1.
Bao la Tambaza Youth limefungwa na Noel Hagaya dakika 31 kipindi cha kwanza na bao la kusawazisha la Tandika United limefungwa na Gwiji Mageuzi dakika ya 72.
Tambaza Youth ambao ni mabingwa wa fainali hiyo amekabidhiwa kombe , medali na fedha pia imetoa nyota bora wa mchezo Noel Hagaya, kipa Bora Amir Seif na kocha bora Mwinyimadi Tambaza.
Tandika United ni washindi wa pili wamepata zawadi ya Jezi na Mipira pamoja na medali, pamoja na kutoa mchezaji bora wa fainali hiyo ambaye ni Gwiji aliyefunga bao la kusawazisha la Tandika.
Mgeni rasmi wa fainali hiyo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania, Almasi Kasongo ambaye amewapongeza DRFA kwa kuandaa mashindano hayo na kusema kuwa anaimani soka la vijana ni sehemu kubwa ya kujenga timu bora ya taifa viongozi wa juu wanapambania.
Nae Mwenyekiti wa DRFA, Lameck Nyambaya amesema anawapongeza Tambaza Youth kwa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo na kusema kuwa DRFA itaendelea kuandaa mashindano mengine kama hayo ili kukuza mchezo.
“Hatutaishia katika mashindano hayo ya U-17 bali tunaendelea na mashindano mbalimbali ya vijana, watu wa mkoa wa Dar es Salaam wajiandae na kuandaa timu zao,” amesema Nyambaya.




