
KLABU ya Simba imefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba na Kocha Mkuu, Zoran Maki.
Taarifa ya Klabu hiyo iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez imesema vile vile Simba imefikia makubaliano ya kusitisha mikataba ya Kocha wa viungo Sbai Karim na Kocha wa Makipa Mohammed Rachid.
“Tayari mchakato wa haraka wa kutafuta makocha wapya umeanza na unatarajiwa kukamilika hivi punde,” imesema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kuelekea mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania bara Septemba 7 dhidi ya KMC kikosi cha Simba kitakuwa chini ya Kocha msaidizi Selemani Matola.
Zoran alisaini mkataba wa mwaka mmoja Simba na kutambulishwa rasmi Julai 12, 2022 akichukua mikoba ya Pablo Franco aliyetimuliwa kabla.