JKT yapania kurudi Ligi Kuu
KATIBU wa JKT Tanzania, Abdul Nyumba amesema kuwa baada ya kuboresha benchi lao la ufundi kwa kumpa mkataba kocha Malale Hamsini, lengo lao ni kuhakikisha timu hiyo ina panda Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24.
Tayari maafande hao wa JKT Tanzania wamekamilisha usajili na kuboresha kikosi chao kwa ajili ya msimu mpya wa 2022/23 wa Championship unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 17, 2022.
Akizungumza na gazeti la HabariLEO, Nyumba amesema wamefanya maboresho makubwa kwenye benchi la ufundi kwa kuachana na Kocha Mohamed Baresi na kumpa mkataba Malale kukinoa kikosi cha timu hiyo kwa lengo kubwa kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
“Msimu huu tumejipanga kurejea rasmi katika Ligi Kuu kwa sababu tumefanya usajili wa wachezaji wenye uwezo mkubwa na kufanya pre season, tunatarajia msimu huu, hatutaki kucheza play-off,” amesema Nyumba.
Amesema katika kufikia malengo hayo wamefanikiwa kumpa mahitaji yote, ikiwemo usajili wa wachezaji 10 wapya ambao wamewahi kucheza katika timu za ligi Kuu ikiwemo Mtibwa na KMC FC.
Wachezaji waliosajiliwa na timu hiyo ni Hassan Kapalata, Emmanuel Kichiba, Ally Yusuph,
Riphat Msuya, Mohammed Katoto, Maka Edward, Maulid Juma, Richard Jovit, Siraji Juma na Hidim Yusuph.




