Jordan Henderson kupiga ‘Jackpot’

KIUNGO Jordan Henderson amepewa ofa ya dili lenye thamani ya kitita cha pauni 700,000 sawa na shilingi bilioni 2.1 kwa wiki ili kujiunga na klabu ya Al-Ettifaq ya Saudi Arabia.
Nahodha huyo wa Liverpool wakati wowote atakuwa na mazungumzo na kocha Jürgen Klopp kujua hatma yake Anfield lakini ni matarajio yake kuungana na Steven Gerrard ambaye hivi karibuni ameteuliwa Kocha wa Al-Ettifaq.
Henderson bado ana miaka miwili iliyobaki kwenye mkataba wake Anfield unaoaminika kuwa na thamani ya pauni 190,000 kwa wiki lakini Al-Ettifaq inakusudia kumsajili na kuwa tayari kuongeza mara tatu mshahara wake.
Al-Ettifaq ya mji wa Dammam pia italazimika kuilipa Liverpool kiasi kikubwa cha ada ya uhamisho.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33 anafahamu nia ya Al-Ettifaq kwa zaidi ya wiki mbili sasa na hakuna swali nia hiyo imempa uamuzi mkubwa wa kufanya.
Henderson anatamani kuwa katika sehemu ya juhudi za Liverpool za kuwapa changamoto Manchester City kwa mara nyingine tena lakini hana uhakika kwamba atakuwa akianza kwenye mechi.
Klopp amewasajili Alexis Mac Allister na Dominik Sbozoszlai kuboresha safu ya kiungo majira haya ya joto na alimchezesha Trent Alexander-Arnold nafasi hiyo kuelekea mwisho wa msimu uliopita.