Tetesi

Mbappé pasua kichwa PSG

KYLIAN MBAPPÉ ameambiwa kwamba ni lazima asaini nyongeza ya mkataba katika klabu ya Paris Saint-Germain ifikapo Julai 31 vinginevyo timu hiyo itajaribu kumuuza majira haya ya joto.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake wa sasa Parc des Princes na mwezi uliopita amepeleka barua kwa uongozi wa klabu akieleza kwamba hataongeza mkataba kusalia kwa mabingwa hao wa Ligue 1.

Hatua hiyo imezua tetesi nyingi za uhamisho huku Real Madrid ‘Los Blancos’ iliyokuwa na nia naye kwa muda mrefu ikianza mara moja kusaka saini ya Mbappé mwenye umri wa miaka 24.

Hata hivyo, tayari Los Blancos imemsajili Jude Bellingham kwa Euro milioni 103 sawa na shilingi bilioni 262.88 majira haya ya joto na imeripotiwa inaamini kwamba Vinicius Junior ana kipaji zaidi ya Mbappé na haitaki kukwamisha maendeleo ya mbrazil huyo.

Lakini kuondoka kwa Karim Benzema kwenda Saudi Arabia kumeacha pengo katika safu ya ushambuliaji ya Real ambayo inaweza kuzibwa na Mbappé iwapo timu hiyo itaamua kuhitaji saini yake majira haya ya joto.

Bisha shaka, mfaransa huyo angeweza kuhamia Santiago Bernabeu msimu uliopita wakati mkataba wake PSG ulipomalizika 2022 lakini alichagua kuongeza miaka miwili zaidi kukiwa na chaguo la kuongeza mwaka wa tatu ambao ni lazima auhuishe yeye mwenyewe.

Kwa mujibu wa mtandao wa michezo wa kifaransa, L’Equipe, PSG imemwambia Mbappé kwamba ni lazima aamue kubaki klabu hiyo kabla ya Agosti vinginevyo itatafuta namna ya kumwondoa dirisha hili la usajili.

Awali nyota huyo alisisitiza kwamba angependa kubaki klabu hiyo lakini hataki kuwepo PSG zaidi ya mwaka ujao.

Hata hivyo, sasa PSG imeripotiwa iko tayari kumuuza fowadi huyo majira haya ya joto kuliko kumpoteza bure mwaka ujao.

Mwaka 2021 PSG ilikataa ofa ya Euro milioni 200 sawa na shilingi bilioni 510.4 kutoka Reala Madrid.

L’Equipe imesema majadiliano kati ya kambi ya Mbappé na PSG yamrejea lakini itachukua muda kufikiwa makubaliano.

Ripoti zimedai PSG inaamini kwamba Mbappé anataka uhamisho huru mwaka 2024 ili apate bonasi kubwa zaidi kutoka klabu itakayomsajili.

Related Articles

Back to top button