FANyumbani

YANGA, AZAM: Nguvu zote FA Tanga

FAINALI ya Kombe la Shirikisho la Azam (FA) inatarajiwa kuhitimishwa Juni 12 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambapo Yanga itachuana na Azam FC.

Safari za mtoano zilianza kwa mabingwa wa mikoa, First League, Championship na timu za Ligi Kuu lakini mwisho wa siku waliotinga hatua hiyo ni hao.

Watu walidhani pengine fainali hiyo ingehusisha Simba na Yanga kutokana na mwenendo wao, lakini safari ya Wekundu wa Msimbazi iliishia hatua ya nusu fainali baada ya kutolewa na Azam FC mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Yanga iliwatoa Singida Big Stars kwa kuwafunga bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Liti, mkoani Singida.

UBORA
Takwimu za Ligi Kuu zinaonesha wazi Yanga ni timu bora na ndio kwanza imetoka kutawazwa kuwa mabingwa mara 29 wa Tanzania Bara.

Ubingwa waliopata msimu huu hawakubahatisha bali ni ubora wa kikosi chao ambacho kimekuwa kikionesha ushindani wa hali ya juu.

Ukilinganisha takwimu zao kwenye ushambuliaji, inaonesha wazi Yanga wamefunga mabao 59 tofauti ya mabao 12 katika michezo 29. Hapo sijahesabu mchezo wa mwisho wa kufunga msimu. Na Azam FC imefunga mabao 47.

Safu ya ulinzi ya Yanga imeruhusu kufungwa mabao 18, machache kuliko ya Azam ni 29. Bado safu ya ulinzi ya Yanga iko vizuri ikiongozwa na kipa wao, Djigui Diarra.

Timu zote mbili zilishiriki michuano ya kimataifa msimu huu lakini Yanga ndio timu pekee ya Tanzania iliyoonesha ubora wa hali ya juu na kufanikiwa kufika fainali ingawa hawakuchukua kombe.

Hatua waliyofika baada ya miaka 30, kwa maana mara ya mwisho ni Simba ilifika, ni kubwa na imedhihirisha namna walivyo vizuri huku wakitoa mfungaji bora, Fiston Mayele aliyefunga mabao saba na mchezaji bora wa mechi ya fainali Diarra.

Yanga kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika ilifungwa na USM Alger ya Algeria nyumbani 2-1 na ugenini ikashinda bao 1-0. Hivyo, wenzao walichukua kombe kwa mabao mengi ya ugenini.

Timu hiyo ya Jangwani imeonesha uchu wa kutaka Kombe hilo la FA ili kuweka rekodi nyingine ya kutwaa kombe la pili mfululizo. Msimu uliopita walichukua.

KUKUTANA
Yanga na Azam FC zimeshakutana mara nyingi. Lakini zaidi msimu huu ni mara mbili na kuchukua pointi nne kutoka kwa wanalambalamba hao wa Chamazi. Mchezo wa kwanza walitoka sare ya mabao 2-2 kisha ule wa marudiano Yanga ilishinda mabao 3-2.

Ulikuwa ni mchezo wenye ushindani huku kila timu ikionesha mapambano ya hali ya juu ingawa mwisho wa siku kuna mmoja alikuwa ni zaidi ya mwenzake. Ukiacha takwimu hizo za kwenye ligi, pia, waliwahi kukutana kwenye fainali ya FA msimu wa mwaka 2015/2016 na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

MECHI YA KESHOKUTWA
Mshindi wa michuano hiyo imezoeleka anawakilisha nchi katika michuano ya kimataifa kwa
maana ya Kombe la Shirikisho Afrika. Lakini tayari timu zote zimeshafuzu michuano ya
kimataifa kwani Tanzania itawakilishwa na timu nne baada ya Yanga na Simba kufanya vizuri na kuongeza pointi nyingi katika nchi.

Kwa maana hiyo, Azam FC kwa kuwa ina ukame wa mataji inataka isimalize msimu bure, imedhamiria kupambana kuchukua kombe hilo kwa ajili ya kuweka heshima. Timu hiyo hata kama haitachukua kombe tayari ilikuwa kwenye nne bora ambazo zilipewa nafasi
ya kushiriki michuano ya kimataifa isipokuwa wanahitaji heshima.

Mara ya mwisho Azam FC kuchukua taji la FA ilikuwa msimu wa mwaka 2018/2019 na imechukua mara moja tu kama ilivyowahi kuchukua ligi mara moja. Yanga imechukua kombe hilo mara mbili kwa hiyo ikifanikiwa kuchukua tena itafikia rekodi ya Simba anayeongoza kwa kuchukua mara tatu.

Yanga sio kwamba wanalitaka kombe hilo ili wapate nafasi ya kimataifa, tayari wao ni mabingwa wa ligi wameshafuzu ila wanataka kuweka rekodi nyingine ya mataji. Kutokana na umuhimu huo kwa maana ya heshima na rekodi hakika haitakuwa mechi rahisi kwa kila mmoja bali unaweza kuwa mchezo mgumu.

Lakini atakayechukua taji ni yule ambaye atakuwa amejiandaa vizuri dhidi ya mpinzani wake kimbinu. Kwa sababu kila timu ina wachezaji wazuri. Bila kujali nani ni bora kuliko
mwingine linapokuja suala la fainali mambo mara nyingi yanaweza kugeuka kwa sababu ni mechi ya kombe kwa hiyo wachezaji pande zote mbili watacheza kwa ubora wa hali ya juu kupata kile walichokidhamiria.

HATARI
Bado unaweza kusema kila upande una wachezaji wake hatari na kwa Yanga Fiston Mayele
na Kennedy Musonda wanapaswa kuogopwa kwa kuwa ni wachezaji wazuri na wameonesha
kiwango kizuri katika mashindano tofauti.

Related Articles

Back to top button