
TIMU ya soka ya Namungo imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ihefu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Bao pekee la Namungo lilifungwa na Reliants Lusajo dakika ya 49 lililodumu hadi kumalizika kwa mchezo huo.
Ushindi huo unaifanya Namungo kufikisha pointi nne baada ya kucheza michezo miwili, kushinda mmoja na kupata sare moja, huku mchezaji wake Lusajo akiwa katika kiwango bora baada ya kufunga jumla ya mabao matatu katika michezo miwili.
Katika mchezo uliopita Namungo ililazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mtibwa Sugar, ambapo Lusajo alifunga mabao yote mawili kwa timu yake.
Aidha, hali ni mbaya kwa Ihefu ambao wanapoteza mchezo wa pili mfululizo baada ya kutoka kupoteza mchezo wa kwanza bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting.
Awali, katika mchezo huo timu zote ziliingia zikiwa makini zikishambuliana kwa zamu lakini pia, kila mmoja akilinda lango lake vizuri hali iliyopelekea kwenda mapumziko ya kipindi cha kwanza wakiwa hawajafungana.
Kipindi cha pili Namungo iliingia kwa kasi na kutengeneza nafasi moja iliyotokana na makosa ya timu pinzani na kufanikiwa kufunga bao hilo, ingawa ilikuwa na nafasi ya kuondoka na ushindi zaidi kama ingekuwa makini.
Ihefu baada ya kufungwa walianza kushambulia langoni la wapinzani ila walichelewa wenzao walikuwa makini kulinda ushindi wao.