MICHUANO YA CAF: Simba, Yanga kutafuta heshima, historia

WEKUNDU wa Msimbazi, Simba na Yanga wana kibarua kizito wikiendi hii katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika wakitafuta matokeo mazuri katika michezo ya hatua ya robo fainali.
Simba itacheza leo dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa, Wydad Casablanca ya Morocco kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, huku Yanga Aprili 23 ikiwa ugenini dhidi ya Rivers United ya Nigeria.
SIMBA VS WYDAD
Simba awamu hii imekuwa na bahati ya kukutana na timu za Morocco, kwenye hatua ya makundi ilicheza na Raja Casablanca ambao wekundu hawakuambulia pointi katika michezo miwili ya nyumbani na ugenini.
Simba ilitinga hatua ya robo fainali baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi C ikiwa na pointi tisa nyuma ya vinara Raja walioingia kwa pointi 16 huku Horoya ya Guinea
ikimaliza ya tatu kwa pointi saba na Vipers ya Uganda ikiwa ya mwisho kwa pointi mbili.
Wekundu hao wa Msimbazi kuingia kwao robo fainali haikuwa jambo jipya kwa kuwa huu ni mwaka wa nne wanafanya vizuri hivyo wanatafuta historia mpya ya kufanya vizuri na kutinga hatua ya nusu fainali.
Kwa upande wa Wydad ni miongoni mwa timu bora za Afrika kwa sasa, kwanza wanatafuta nafasi ya kutetea taji lao.
Wydad ilikuwa kwenye Kundi A ikimaliza kwa kuongoza hatua ya makundi kwa pointi 13, wengine wakiwa ni JS Kabylie ya Algeria ikiwa ya pili kwa pointi 10, Petro de Luanda pointi saba na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwenye hatua ya makundi, Wydad walicheza michezo sita na kati ya hiyo, walipoteza mmoja, sare moja na kushinda michezo minne kwa hiyo sio timu ya kubeza. Simba katika idadi hiyo ya mechi, ilishinda mitatu na kupoteza michezo mitatu.
Mchezo huu wa leo unaweza kuwa mgumu kwa wekundu kwa sababu wanakutana na timu yenye rekodi nzuri kwenye michuano ya Afrika.
Timu za Kiarabu mara nyingi zinapokuwa ugenini zinacheza kwa kupooza, kupoteza muda kana kwamba hawana presha lakini wakipata nafasi wanajua kuzitumia. Ugenini hata wakipata sare ni matokeo mazuri kwao kwa sababu wanaamini watakwenda kumaliza kwao.
Lakini pamoja na ubora walionao Wydad haimaanishi kwamba Simba iwaogope bali wajipange na kuwa imara kuhakikisha wanamaliza kazi nyumbani kwani lolote linawezekana.
Simba kwa siku za karibuni imeonesha soka zuri, wachezaji wana morali hasa baada ya kutoka kushinda mchezo wao uliopita dhidi ya Yanga mabao 2-0. Ushindi huo unamaanisha
kwamba wako tayari kupambana na Wydad na wanaamini wanaweza kupata matokeo mazuri.
Iwapo Simba itashinda mchezo huo wa robo fainali na kuvuka hatua inayofuata itaandika rekodi ya kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu kuanzishwa kwake. Wakati wapinzani wao, Wydad rekodi zao kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wametwaa taji hilo mara tatu mwaka 1992, 2017 na 2021/22.
Mafanikio mengine wamecheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa mara sita mwaka 1992, 2017, 2016, 2019/20, 2020/21 na 2022/23, kitu kinachofanya mchezo uonekane mgumu
kwa pande zote mbili.
Moja kati ya rekodi za kusisimua kwa Simba ni mwaka 2003 ambapo waliwatoa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Zamalek kwa mikwaju ya penalti na kutinga hatua ya
16 bora.
Simba ilianza kushinda kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru kabla ya kwenda kupoteza ugenini bao 1-0 lakini ikasonga mbele baada ya kuibuka na ushindi kwa njia ya mikwaju ya penalti 3-2.
Rekodi hii ya kumtoa bingwa mtetezi inaweza kutokea tena msimu huu iwapo kama Simba itachanga vyema karata zake inaweza kucheza nusu fainali yake ya kwanza.
YANGA VS RIVERS UNITED
Yanga ina bahati ya kukutana na Rivers baada ya mwaka juzi kukutana na kupoteza michezo yote miwili kila mmoja bao 1-0 nyumbani na ugenini. Ni mchezo ambao Yanga
wanaamini wanaweza kulipiza kisasi kwa sababu kipindi kile walivyokutana hawakuwa vizuri hivyo kwa sasa wana ubora.
Yanga imemaliza Kundi D ikiwa kinara kwa kufikisha pointi 13 baada ya kucheza michezo sita, kushinda minne, sare moja na kupoteza moja.
Ni rekodi ya kipekee wameiweka msimu huu ukilinganisha na miaka mingine waliyowahi kufika hatua ya makundi huko nyuma ambako walikuwa wanafungwa sana na hata kumaliza kundi katika nafasi ya tatu na nne.
Mshindi wa pili alikuwa ni US Monastir ya Tunisia waliolingana pointi, wakifuatiwa na Real Bamako ya Mali yenye pointi tano na TP Mazembe ikishika mkia kwa pointi tatu.
Rivers United ilikuwa Kundi B na ilimaliza katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 10 nyuma ya vinara, Asec Mimosas ya Ivory Coast iliyokuwa na pointi 13. Katika michezo sita waliyocheza walishinda mitatu, sare moja na kupoteza miwili.
Walikuwa na Diables Noirs ya Congo iliyokuwa katika nafasi ya tatu kwa pointi sita na Motema Pembe ya DRC pointi tatu.
Takwimu za timu hii zilipokuwa kwenye uwanja wa nyumbani wameonesha walikuwa moto na wala hawapaswi kubezwa walishinda mabao 3-0 dhidi ya Asec Mimosas, wakashinda mabao 3-1 dhidi ya Motema Pembe na kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Diables Noirs.
Rivers walishinda mechi moja ya ugenini bao 1-0 dhidi ya Motema Pembe. Pamoja na uchanga wao kwenye michuano ya Afrika ni timu ambayo inajitahidi kwa kiasi fulani.
Rekodi zao zinaonesha timu hiyo iliyoundwa mwaka 2016, imeshiriki Ligi ya Mabingwa mara mbili mwaka 2017 ilitolewa hatua za awali na mwaka 2022 ilitolewa raundi ya pili.
Mwaka 2017 baada ya kutolewa raundi za awali, waliangukia kwenye Kombe la Shirikisho na kufanikiwa kuishia hatua ya makundi ikiwa bado ni timu changa kwa hiyo hayo yalikuwa
mafanikio makubwa kwao.
Mwaka 2020/2021 walitolewa kwenye mchezo wa mwisho wa mtoano na kushindwa kuingia hatua ya makundi.
Msimu huu wamevunja rekodi kwa sababu ni mara ya kwanza wanaingia hatua ya robo fainali ikionesha dhahiri na wao wanataka mafanikio zaidi na wamejitahidi hadi hapo walipofikia wakionesha ushindani kwa timu kongwe walizocheza nazo hatua ya makundi.
Rivers ni kama Yanga walianzia Ligi ya Mabingwa wakatolewa kwenye mtoano na kuangukia Kombe la Shirikisho.