Majaliwa ataka michezo ipewe kipaumbele

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa rai kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha sekta ya michezo inaendelea kupewa kipaumbele katika ngazi zote hapa nchini.
Majaliwa ametoa raia hiyo bungeni jijini Dodoma leo wakati wa kuipongeza timu ya Fountain Gate ya wasichana iliyotwaa ubingwa wa Soka Afrika kwa upande wa Shule za Sekondari hivi karibu Afrika Kusini.

“Naupongeza uongozi wa shule hii pamoja na Alliance ya jijini Mwanza kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuunga mkono maendeleo ya Sekta ya Michezo nchini, tunawashukuru sana naamini mtaendelea kufanya hivyo katika michezo mingine” Amesisitiza Mhe. Majaliwa.
Awali, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Wizara itaendelea kuratibu mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwa kuwa ni miongoni mwa mashindano yanayozalisha wachezaji wengi.