Antonio Conte akalia kuti kavu
KOCHA wa klabu ya Tottenham Hotspur ya Ligi Kuu England, Antonio Conte amekiri anaweza kutimuliwa kazi hata kabla ya kupata nafasi ya kufikia uamuzi wa mwisho wa hatma yake katika klabu hiyo.
Mkataba wa Conte unamalizika mwisho wa msimu huu na ingawa Spurs ina chaguo la kuuongeza kwa mwaka mmoja zaidi, habari zinasema kuna makubaliano ya pande zote kuwa kuachana na kocha huyo itakuwa bora zaidi kwa kila pande inayohusika.
Hata hivyo, baada ya Spurs kuondolewa Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya AC Milan, Conte amekiri kwamba hatafika mwisho wa msimu.
“Mkataba wangu unamalizika Juni. Tutaona-wanaweza kunitimua hata kabla ya mwisho wa msimu, hakuna anayejua, labda wamekata tamaa,” amekiri Conte.
Kuna habari kwamba Kocha wa zamani wa Spurs Mauricio Pochettino anaweza kurejea klabu hiyo iwapo Conte ataondoka.




