Nandy amjibu Zuchu, ataka mumewe Billnass aheshimiwe

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Faustina Mfinanga ‘Nandy’, amevunja ukimya na kumjibu msanii mwenzake Zuhura Othuman ‘Zuchu’ kufuatia tuhuma na kauli mbalimbali zilizotolewa dhidi yake, ikiwamo madai ya kuiga mambo anayofanya Zuchu.
Nandy amesema hakupenda kuingia katika majibizano na Zuchu, lakini amelazimika kutoa ufafanuzi ili kuweka mambo sawa, hususan kuhusu suala la pete mpya za ndoa alizonunua pamoja na mumewe, rapa Billnass.
Awali, Zuchu alidai kuwa baada ya mpenzi wake, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, kumnunulia pete na cheni za dhahabu, Nandy naye alienda kununua pete mpya za ndoa pamoja na mumewe na kutafuta kiongozi wa kiroho kwa ajili ya kuziombea.
Akijibu madai hayo, Nandy amesema ununuzi wa pete hizo haukuhusiana na ushindani wowote, bali ulitokana na kupotea kwa pete zao za awali walipokuwa safarini pamoja na mumewe.
Amesema pete walizokuwa nazo awali zilikuwa na thamani kubwa zaidi, lakini zilipotea baada ya kurejea nyumbani kutoka safari wakiwa wamefika usiku wa manane.
Kwa mujibu wa Nandy, walipoamka asubuhi iliyofuata walibaini kuwa pete hizo hazikuwepo, huku dereva wao akiwa amechukua gari kwenda kulisafisha na aliporejea hawakuweza kuzipata tena, hali iliyowalazimu kununua nyingine.
Mbali na suala la pete, Nandy ameonekana kukerwa pia na kauli za Zuchu zinazomhusisha mumewe, Billnass, baada ya kudai kuwa amepata mume wa kumhangaisha.
Akizungumzia suala hilo, Nandy amemtaka Zuchu kumheshimu mumewe na ndoa yake, akisisitiza kuwa Billnass hana tatizo na mtu yeyote na hastahili kuingizwa katika mvutano huo.
Amesema yeye mwenyewe amekuwa akimheshimu Diamond Platnumz na hajawahi kuzungumzia vibaya uhusiano au ndoa ya Zuchu, huku akieleza kuwa hata Billnass anamheshimu Diamond.
Kutokana na hali hiyo, Nandy amesisitiza kuwa heshima inapaswa kuwa ya pande zote, akimtaka Zuchu kuacha kumhusisha mumewe katika kauli zinazoweza kuleta tafsiri tofauti kwa mashabiki.
Majibizano hayo yanaendelea kuvuta hisia za mashabiki wa Bongo Fleva, hasa kutokana na ukweli kwamba wasanii hao wawili wamekuwa wakihusishwa na ushindani wa kimuziki kwa muda mrefu.




