Kwingineko

Mwanamuziki mkongwe akutana na Papa Leo XIV mjini Vatican

VATICAN: MWANAMUZIKI mkongwe kutoka Marekani, Bob Dylan, amekutana na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, katika ziara yake mjini Vatican, Italia,

Wawili walipokutana wamebadilishana zawadi katika tukio lililovutia wadau wa muziki na watu mbalimbali duniani.

Katika mkutano huo, Dylan alimkabidhi Papa Leo XIV kitabu chake kinachoelezea maisha yake, huku kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki akimkabidhi mwanamuziki huyo rozari kama zawadi ya kumbukumbu ya kukutana kwao.

Dylan, ambaye ni miongoni mwa wanamuziki wenye ushawishi mkubwa katika historia ya muziki wa kimataifa, amejijengea jina kupitia nyimbo zake zenye ujumbe wa kijamii, kisiasa na maisha ya kila siku.

Umaarufu wa mwanamuziki huyo ulianza kushika kasi katika miaka ya 1960 kupitia nyimbo zilizogusa masuala ya haki za binadamu na amani.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 85 pia aliandika historia mwaka 2016 baada ya kutunukiwa Tuzo ya Nobel ya Fasihi kutokana na mchango wake katika utunzi wa mashairi na nyimbo, akitajwa kwa kuibua namna mpya ya kujieleza kishairi kupitia muziki.

Kwa upande wake, Papa Leo XIV ameendelea kupokea wageni mbalimbali kutoka sekta tofauti za maisha, wakiwemo viongozi, wanamichezo na watu mashuhuri, katika shughuli zake za kidini na kijamii mjini Vatican.

Kukutana kwa Dylan na Papa Leo XIV kumeonesha nafasi ya muziki katika kuunganisha watu wa tamaduni na imani tofauti, huku tukio hilo likiwa kumbukumbu nyingine katika maisha ya mwanamuziki huyo ambaye amedumu katika tasnia ya muziki kwa zaidi ya miongo sita.

Related Articles

Back to top button