Filamu

Bodi ya filamu yawataka wasanii kuzingatia utaratibu wa usambazaji

DAR ES SALAAM: BODI ya Filamu Tanzania imeipongeza Kampuni ya Umoja Movies Distribution kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usambazaji wa filamu nchini, ikiwemo kuwasilisha kazi za filamu wanazozisambaza kwa ajili ya kuhakikiwa na Bodi hiyo.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Filamu wa Bodi ya Filamu Tanzania, Emmanuel Ndumukwa, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za Bodi hiyo, ukihusisha pia wawakilishi wa Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA).

Ndumukwa amesema Umoja Movies Distribution imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia miongozo iliyowekwa, hatua inayosaidia kuhakikisha shughuli za usambazaji wa filamu zinafanyika kwa utaratibu na kwa mujibu wa sheria.

Amesema ni muhimu kwa kampuni na wadau wengine wanaojihusisha na usambazaji wa filamu kujifunza kutoka kwa kampuni hiyo kwa kujirasimisha na kuendesha shughuli zao kwa uwazi badala ya kufanya biashara hiyo kwa kificho.

Aidha, amesisitiza kuwa maelekezo ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Naibu Waziri, Hamis Mwinjuma, ni kuendelea kuchukua hatua dhidi ya uharamia wa kazi za filamu na michezo ya kuigiza.

Amesema uharamia unaathiri uchumi wa wasanii kwa kuwanyima manufaa yanayotokana na kazi zao za ubunifu, huku watu wachache wakinufaika na kazi zinazozalishwa na wasanii wengi.

Kwa upande wake, Afisa Hakimiliki Mkuu wa COSOTA, Paul Makula, ametoa mwongozo kwa wadau wa filamu kuhusu taratibu za kuzingatia katika masuala ya hakimiliki.

Makula amesema ni muhimu kuhakikisha matumizi na usambazaji wa kazi za wasanii vinafanyika kwa kuzingatia haki za wamiliki wa kazi hizo ili kulinda maslahi yao na kuwapa nafasi ya kunufaika na ubunifu wao.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usimamizi wa sekta ya filamu nchini, kulinda hakimiliki na kuhakikisha wadau wote wanafanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Related Articles

Back to top button