Amitabh Bachchan atinga na kioo cha kuzuia risasi

MUMBAI: Katika hali isiyo ya kawaida, mwigizaji mkongwe, Amitabh Bachchan amesalimiana na mashabiki zake akiwa kwenye kioo cha kuzuia risasi.
Video iliyosambaa mitandaoni, imemuonesha mkongwe huyo akiwa kwenye kioo hicho nje ya nyumba yake, Jalsa huko Juhu akiendelea na utaratibu wa kusalimia mashabiki zake kila Jumapili.
Aidha, mtoto wa Amitabh, Abhishek Bachchan pia alikuwepo kufuatilia hali ya usalama, kama ilivyokuwa kwa Polisi wa Mumbai waliokuwepo eneo hilo.
Hayo yanaibuka baada ya tukio la Oktoba 18, mwaka huu ambapo mwigizaji, Tiger Shroff akiwa Juhu, gari yake ilishambuliwa kwa risasi alipokuwa akirudi kuangalia mechi ya mpira wa miguu.
Kama haitoshi, Oktoba 23, ujumbe wa vitisho ulitumwa kwa Meya wa Mumbai, Ritu Tawde na kwa Naibu Meya, Sanjay Ghadi, ikitaja makazi ya Amitabh, ofisi ya meya na ukumbi wa tamasha lijalo la mwimbaji, Diljit Dosanjh huko Mumbai.

Ujumbe huo wa barua pepe, zaidi umeonya kuhusu shambulio huko Jalsa kati ya Oktoba 31 na Novemba 27, mwaka huu.
Aidha, wakati wa salamu zake za Jumapili, Amitabh, 84 alizungumzia hali yake ya afya: “Bado nahitaji kupumzika zaidi, kujirekebisha, kutafakari na kujiuliza kuhusu mwili wa binadamu na namna ulivyo wa kipekee.”
Kwa sasa Amitabh anaongoza msimu wa 18 wa Kipindi cha Kaun Banega Crorepati. Mara ya mwisho alionekana katika filamu ya Vettaiyan ya mwaka 2024, akiwa pamoja na Rajinikanth.




