Burudani

Tanzania Comedy Festival kufanyika Novemba 27 Mlimani City 

DAR ES SALAAM: TANZANIA Comedy Festival inatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2026, katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam,

Ikiwa ni sehemu ya kuwakutanisha Watanzania pamoja kupitia burudani ya vichekesho na kufunga mwaka kwa furaha.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya tamasha hilo, Mratibu wa Tanzania Comedy Festival, Frank Mathew, amesema kuwa baada ya shughuli na pilikapilika za mwaka mzima kuanzia Januari hadi Novemba, sasa ni wakati wa Watanzania kukutana pamoja, kufurahi na kucheka.

Katika kuelekea tamasha hilo, Novemba 12, 2026, kutakuwa na mechi ya hisani kati ya wachekeshaji na timu ya Azam Media.

Mapato yatakayopatikana kupitia mchezo huo yatatumika kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, wakiwemo watoto wenye changamoto ya midomo sungura.

Aidha, tamasha hilo litaambatana na shughuli za kijamii, ikiwemo kutoa misaada katika vituo vya watoto yatima kwa lengo la kuwapa faraja na kuwashika mkono watu wenye uhitaji.

Tamasha hilo litapambwa na wachekeshaji mbalimbali maarufu, akiwemo Deogratius Kimboya, Leyla Manga, Bobindo na Teacher Professor Kashasha, pamoja na wengine wengi.

Kwa upande wake, Mshehereshaji Kisori amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kushuhudia kile kilichoelezwa kuwa usiku wa kipekee wa vicheko na burudani ya mwaka.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Azam Media, Yahya Kimaro, amesema kuwa licha ya changamoto mbalimbali zilizopitiwa katika kipindi cha mwaka, tamasha hilo ni fursa ya kukutana, kufurahi na kucheka pamoja kama Watanzania.

Akizungumzia maandalizi ya burudani hiyo, Mkuu wa Chaneli ya Sinema Zetu, Sophia Mgaza, amesema wameandaa burudani maalumu ya kufunga mwaka itakayowasaidia watu kupumzika kutoka katika changamoto za maisha na kuukaribisha mwaka mpya kwa furaha na vicheko.

Kwa upande wake, Afisa Mawasiliano wa Azam, Tina Koroso, amesema timu ya soka ya Azam TV ipo tayari kwa mchezo wa hisani dhidi ya wachekeshaji, huku akiwataka wachekeshaji hao kujiandaa kukabiliana na ushindani wa uwanjani.

Tanzania Comedy Festival inatarajiwa kuwa jukwaa la kuunganisha burudani, mshikamano na shughuli za kijamii, huku Watanzania wakipata nafasi ya kufunga mwaka 2026 kwa kucheka na kufurahia pamoja.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button