Michezo Mingine

Hamilton: Fomula 1 haijawahi kuwa na dereva kama mimi

BINGWA mara saba wa dunia wa mashindano ya magari ya Formula 1, Lewis Hamilton, amesema hakuna dereva aliyewahi kufanana naye katika historia ya mchezo huo, akisisitiza kuwa bado ana uwezo wa kuendelea kushindana hadi kufikia umri wa miaka 45 na kuendelea.

Hamilton, mwenye umri wa miaka 41, amesema hana mpango wa kustaafu hivi karibuni, huku akieleza kuwa bado ana ari na dhamira ya kuendelea kushiriki mashindano hayo katika kiwango cha juu.

Dereva huyo wa timu ya Ferrari amekuwa akitamani kushiriki mashindano ya Formula 1 barani Afrika, ndoto ambayo ameipigania kwa miaka mingi. Matumaini hayo yameongezeka baada ya F1 kusaini mkataba wa miaka 10 na Rwanda kuandaa mashindano hayo kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 2030.

Akizungumza kuelekea mashindano ya Mexican Grand Prix, Hamilton alisema Formula 1 haijawahi kuwa na mtu kama yeye katika historia yake ya miaka 70, akiamini kuwa uwezo wake wa kipekee unamtofautisha na madereva wengine.

Alipoulizwa kuhusu athari za umri katika uwezo wa dereva, Hamilton alieleza kuwa changamoto za uzee haziwezi kuepukika, lakini bado ana kasi nzuri ya kufanya maamuzi na mwitikio wa haraka, akitolea mfano wa kiwango alichoonyesha katika mashindano yaliyopita.

Kwa sasa, Hamilton anapambana kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa madereva msimu huu, akichuana na madereva wengine wanne nyuma ya Kimi Antonelli wa Mercedes, ambaye anaongoza kwa tofauti kubwa. Baada ya kupitia msimu mgumu katika mwaka wake wa kwanza Ferrari, amerejea kwa kiwango kizuri zaidi, ikiwemo ushindi wa Barcelona-Catalunya Grand Prix mwezi Juni.

Hata hivyo, Hamilton amesema ataendelea kushindana kwa kuwa bado ananguvu ya kufanya hivyo, akisisitiza hataki kuendelea na mchezo huo pale ambapo kiwango chake kitakuwa kimeshuka.

Amesema bado ana dhamira ya kuthibitisha kuwa umri si kikwazo cha mafanikio.

Related Articles

Back to top button