EPL

Neville: Kufukuzwa makocha ni jambo jema kwao

ENGLAND: ALIYEKUWA nahodha wa Manchester United, Gary Neville, amesema wakati mwingine kufutwa kazi kwa makocha kunaweza kuwa jambo jema kwa makocha wanaopitia wakati mgumu.

Wakati Neville akitoa kauli hiyo kocha wa sasa wa klabu hiyo, Michael Carrick, anaendelea kukabiliwa na presha kubwa kutokana na matokeo mabaya ya timu.

Mustakabali wa Carrick katika klabu hiyo umeendelea kuwa mjadala mkubwa baada ya Manchester United kukaa mechi nane mfululizo bila kupata ushindi. Hali hiyo ilizidi kuwa mbaya baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-0 nyumbani dhidi ya Bournemouth Jumapili iliyopita.

Matokeo hayo yameiacha Manchester United ikiwa na tofauti ya pointi moja pekee juu ya eneo la kushuka daraja katika msimamo wa Ligi Kuu England, hali inayoonesha ukubwa wa changamoto inayokikabili kikosi hicho.

United imefanikiwa kushinda michezo miwili pekee kati ya 12 katika mashindano yote msimu huu, huku ikikusanya pointi saba katika mechi nane za ligi, ikiwa ni mwanzo wake mbaya zaidi wa msimu ndani ya kipindi cha miaka 40.

Neville, ambaye aliwahi kucheza pamoja na Carrick Manchester United, amesema anaamini viongozi wa klabu hiyo walijadiliana kwa kina kuhusu hatma ya kocha huyo baada ya kichapo dhidi ya Bournemouth, lakini wakashindwa kufikia uamuzi wa kumtimua.

Akizungumza kupitia kipindi cha Stick to Football, Neville alidai kuwa kutokuwepo kwa mipango madhubuti, ukosefu wa makocha mbadala wanaopatikana na kusuasua kwa maamuzi huenda kukawa sababu za klabu kuendelea kumwamini Carrick. Alikumbushia pia uzoefu wake alipokuwa kocha wa Valencia, akisema alifutwa kazi na kuona ni afadhali baada ya kipindi kigumu alichopitia.

Kwa upande wa majina yanayotajwa kuchukua nafasi ya Carrick, aliyekuwa kocha wa Newcastle, Eddie Howe, pamoja na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani, Julian Nagelsmann, wametajwa miongoni mwa wanaoweza kuwania nafasi hiyo. Hata hivyo, Carrick anatarajiwa kuendelea na majukumu yake huku Manchester United ikijiandaa kukutana na Chelsea Jumamosi kesho.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button