Araujo hajui hatima yake Liverpool

LIVERPOOL: BEKI wa Liverpool, Ronald Araujo, amesema bado ni mapema kuzungumzia uwezekano wa kusalia klabuni hapo kwa mkataba wa kudumu, licha ya kuanza vizuri kipindi chake cha mkopo akitokea Barcelona.
Araujo, aliyewahi kuwa nahodha wa Barcelona, amejihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza cha Liverpool akicheza kama beki wa kulia, ingawa nafasi anayopendelea zaidi ni ya beki wa kati.
Liverpool ina fursa ya kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay kwa ada ya pauni milioni 47 (dola milioni 63), lakini bado haijafahamika kama klabu hiyo itatumia kiasi hicho kumsajili kwa kudumu.
Akizungumza kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Villarreal, Araujo alisema bado hajafanya uamuzi kuhusu mustakabali wake, akisisitiza kuwa yeye na familia yake wanafurahia maisha Liverpool.
“Bado ni mapema sana kuzungumzia mambo hayo. Nina furaha kuwa hapa, na familia yangu pia ina furaha,” alisema beki huyo, ambaye tayari ameichezea Liverpool michezo 10.
Araujo alisema kucheza katika klabu kubwa kama Liverpool kunahitaji kujituma, kukabiliana na shinikizo na kutimiza majukumu makubwa, akieleza kuwa uzoefu wake wa Barcelona umemsaidia kuzoea mazingira hayo.
Aliongeza kuwa tangu alipowasili Anfield alijua alipaswa kutoa mchango wake wote kwa timu, akiamini kuwa mafanikio katika klabu kubwa yanahitaji kujitolea na kufanya kazi kwa bidii.
Kwa sasa, mustakabali wa Araujo Liverpool bado haujajulikana, huku kiwango chake katika kipindi kilichosalia cha mkopo kikitarajiwa kuwa muhimu katika maamuzi kuhusu usajili wa kudumu.




