Billnass: Sina ushamba wa kumroga Nandy

DAR ES SALAAM: RAPA Billnass amefunguka kuwa hawezi kutumia ushirikina kumroga mwanamke anayempenda, akitafsiri kufanya hivyo ni ujinga au ushamba.
Hiyo ni baada ya juzi, rapa huyo kueleza awali wakati anauza simu mitaani alikuwa anakamatwa mno na polisi kiasi cha kwenda kwa mganga kuweka mambo sawa lakini haikusaidia.
Sasa anaeleza kuwa hawajawahi kufanya hivyo kwa mkewe, Nandy kwani mapenzi yao yapo na sio ya kuyalazimisha kama yalivyo mengine.
“Ushamba au ujinga wa mapenzi wa namna hiyo sijawahi kuwa nao, sababu hisia ni kitu cha ‘automatically’ haipaswi kulazimisha.
“Upendo ni vile naweza kumtongoza ninaempenda, halafu yeye akawa hanipendi, sasa nikilazimisha anipende inakuwa kiini macho hicho,” alisema Billnass.
Alisema hiyo ni sawa na mtu tajiri aliyeenda kwa mganga aonekane tajiri kwa nje lakini ndani ana mateso ya masharti magumu na mwisho unajidanganya mwenyewe kuhusu uhalisia wa maisha yako.
“Kitu unachoweza kuufanyia moyo wako au kufanya kwenye maisha ni pale unapogundua mpenzi au rafiki ambaye hakuhitaji na kukaa naye mbali.
“Sababu huna namna nyingine ya kufanya zaidi ya kukaa mbali maana ukilazimisha utakuwa mtumwa, sababu huo uchawi ukiisha utakuwa unafanya tena kila baada ya muda au unafanyaje sasa?” Alihoji Billnass.




