Wema Sepetu atoa wito kwa wazazi kuwalinda watoto wa kiume

DAR ES SALAAM:MSANII wa filamu nchini, Wema Sepetu, ametoa wito kwa jamii na wazazi kuongeza umakini katika malezi na ulinzi wa watoto wa kiume, akisisitiza umuhimu wa kuwa karibu nao katika hatua mbalimbali za ukuaji wao.
Wema ametoa ujumbe huo kupitia mitandao ya kijamii, akieleza kuwa watoto wa kiume wanahitaji uangalizi, upendo na malezi bora kutoka kwa wazazi na jamii inayowazunguka.
Kwa mujibu wa Wema, wazazi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao, kuwasikiliza na kuwalea kwa uangalifu ili kuwasaidia kukua katika mazingira salama na yenye maadili.
Ujumbe huo umeibua mjadala katika mitandao ya kijamii, huku baadhi ya watu wakisisitiza kuwa malezi na ulinzi ni muhimu kwa watoto wote bila kujali jinsia.
Wema amesisitiza umuhimu wa jamii kutambua changamoto zinazoweza kuwakabili watoto wa kiume na kuchukua hatua za kuhakikisha wanapata malezi yenye upendo, usalama na mwongozo unaofaa.
Wito huo umeendelea kuchochea mjadala kuhusu nafasi ya wazazi katika malezi ya kizazi cha sasa na umuhimu wa kujenga mazingira ambayo watoto wote wanaweza kukua salama.




