
MSANII wa filamu nchini Burton Mwembe Mwijaku, amekosoa mwenendo wa kipindi cha A-List, akisisitiza kuwa kipindi hicho kinapaswa kulenga kuelimisha na kuburudisha badala ya kuwafedhehesha au kuwaumiza watu wanaohusika.
Mwijaku amemkosoa mwigizaji Kajala Masanja kuhusu namna kipindi hicho kinavyoendeshwa, akidai kuwa baadhi ya maswali yanayoulizwa yanaweza kuathiri utu, hisia na taswira ya watu wanaotajwa.
Kwa mujibu wa Mwijaku, anaelewa kuwa Kajala na wenzake wanafanya juhudi kuhakikisha A-List inapata umaarufu, kuvutia watazamaji na kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, amesema njia inayotumika kufikia malengo hayo inapaswa kuangaliwa kwa umakini, kwani baadhi ya maswali yanaweza kuwa na athari kwa wahusika wanaohusishwa na maudhui ya kipindi.
Mwijaku amedai kuwa baadhi ya maswali yanayoulizwa katika A-List yanaweza kumuumiza au kumvunja moyo msanii Marioo, ambaye ni mkwe wa Kajala.
Kauli hiyo imeibua mneno kwenye mitandao ya kijamii, huku wadau na mashabiki wa burudani wakitoa maoni kuhusu aina ya maswali yanayopaswa kuulizwa katika vipindi vya burudani na mipaka inayopaswa kuzingatiwa katika kutengeneza maudhui yenye kuvutia watazamaji.
Mwijaku amesisitiza umuhimu wa vipindi vya burudani kuwa na maudhui yanayovutia, lakini wakati huohuo yakiheshimu utu na hisia za watu wanaohusika.




