
KOCHA Mkuu wa timu za taifa za wanawake, Bakari Shime amesema licha ya kutwaa ubingwa wa michuano ya Cosafa, hana furaha kwani anakabiliwa na majukumu makubwa ya mechi za kufuzu Afcon kwa Twiga Stars na Kombe la Dunia kwa Tanzanite Queens.
Akizungumza baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nerere (JNIA) wakitokea Afrika Kusini juzi kwenye michuano ya Cosafa, Shime alisema muda waliokaa kambini ni kwa ajili ya mchezo dhidi ya Namibia wa kufuzu Afcon, lakini anafurahi kurudi na kombe.
“Twiga Stars mwezi huu tarehe 20 wana mchezo muhimu dhidi ya Namibia kuwania kufuzu Afcon, sina furaha kwa sababu hili ni jukumu kubwa, muda wote tuliokaa kambini ni kwa ajili ya mchezo huo wa kufuzu Afcon.”
“Tumekuwa mabingwa wa Cosafa na ni jambo nzuri, lakini kule tumepata majeraha wengi na wote ni muhimu kwenye timu na muda uliobaki ni mchache,” aliongeza Shime.
Naye nahodha wa timu hiyo, Amina Ally ambaye ni mchezaji bora wa mashindano ya Cosafa alisema anajisikia furaha kwani siku zinavyozidi kusonga timu yao inaimarika zaidi pia aliishukuru serikali na TFF kwa jinsi ambavyo wamekuwa karibu nao.
“Nafurahi kuwa mchezaji bora kwa kuwashinda wachezaji wengi wa kulipwa kwani wachezaji wengi wa ukanda wa Cosafa ni wa kulipwa, nafurahi na kujisikia fahari kwani kadri siku zinavyozidi kwenda ndivyo timu inavyoimarika,” alisema Amina.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Hassan Abbasi aliongoza mapokezi ya Twiga Stars akiwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Dk Yusuf Singo, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo (BMT), Neema Msitha, viongozi wa TFF na Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka la Wanawake (TWF).
Akizungumza katika tukio hilo, Dk Abbasi aliwaambia wachezaji kuwa serikali itawapa zawadi itakayoonesha thamani ya heshima waliyoliletea taifa kwa kutwaa ubingwa wa Cosafa.
“Siku tunawaaga mliahidi ubingwa leo mmetimiza ahadi yenu sasa kazi iko kwetu kuwaenzi na Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza na ameahidi atawaenzi na kutambua mchango wenu sasa tusubiri ahadi yake,” alisema Dk Abbasi.
Jana jioni serikali ilitarajia kupata chakula cha jioni na wachezaji hao ambapo pia walitarajia kutangaza zawadi zao.