Ligi Daraja La Kwanza

Mwakinyo aingia 10 bora duniani

BONDIA namba moja Tanzania na Afrika katika viwango vya ubora katika uzito wa Super Walter, Hassan Mwakinyo amepanda na kuingia katika orodha ya mabondia 10 bora kati ya 1,530 wanaofanya vizuri katika uzani wake duniani.

Kwa mujibu wa mtandao wa Boxrec, Mwakinyo amepanda kwa nafasi moja kutoka ya 11 hadi kuingia katika orodha ya mabondia 10 bora wa Super Walter duniani, huku akiendelea kuwa na nyota nne.

Katika kipindi cha miaka miwili nyota ya Mwakinyo imezidi kung’ara baada ya kutoka nafasi ya 24, kabla ya kupanda kwa nafasi 11 hadi ya 13 baada ya kuibuka na ushindi mbele ya Julius Ndongo raia wa Namibia na baadae kupanda kwa nafasi mbili hadi 11.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwakinyo alisema anafurahi kuona anazidi kupanda katika viwango vya ubora duniani, kwani hapandi hivi hivi bali ni kutokana na kazi nzuri anayoifanya kwa kushinda mapambano yake.

“Ngumi ni kazi yangu nitaendelea kufanya vizuri kwa kushinda mapambano yangu ili niendelee kupanda katika viwango vya ubora na kuipeperusha vema bendera ya Tanzania kupitia mchezo wa ngumi,” alisema Mwakinyo.

Related Articles

Back to top button